Ibrahim al Wazin, mhadhiri wa chuo cha Qur’ani cha mji wa Tanta nchini Misri ambacho ni kitengo cha Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri amesema kuwa, kuna umuhimu wa kuelewa kwa njia sahihi maana ya aya za Qur’ani Tukufu na tafsiri zake kwa ajili ya kukabiliana na fikra potofu na finyu zinazotumiwa na baadhi ya watu na makundi kuuchafulia jina Uislamu.
Vyombo vya habari vimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, tawi la Taasisi ya Kimataifa ya Wahitimu wa Chuo Kikuu cha al Azhar mkoani Dakahlia kaskazini mashariki mwa Cairo, mji mkuu wa Misri limeitisha warsha na semina maalumu ya kidini kwa ajili ya kutoa ufafanuzi na tafsiri ya baadhi ya aya za Qur’ani Tukufu kwa wanachuo wa Sayansi na Utafiti wa kitengo cha kuhifadhi Qur’ani Tukufu.
Katika hotuba yake, mhadhiri huyo ametoa ufafanuzi kuhusu tafsiri potofu za aya za Qur’ani Tukufu zinazotolewa na baadhi ya makundi yenye misimamo mikali na ya kigaidi kwa ajili ya kuhalalisha jinai zao na kufanikisha malengo yao ya kuupaka matope Uislamu.
Ameongeza kuwa, ni jambo la dharura kuelewa vizuri na kwa njia sahihi maana ya aya za Qur’ani Tukufu kwa ajili ya kukabiliana na madai yasiyo sahihi ya taasisi na makundi yenye misimamo mikali ya kigaidi.
Mhadhiri huyo wa chuo kikuu vile vile amesema, kuwa na ikhlasi katika nia, kuwa na ramani akilini kuhusu sura za Qur’ani Tukufu, kutumia msahafu mmoja na kuelewa makusudio na maana ya sura za Kitabu hicho kitakatifu, ni miongoni mwa njia nzuri za kuhifadhi kwa njia rahisi Qur’ani Tukufu.
Naye Bi Fatma Kishk, msimamiaji wa tawi la Taasisi ya Kimataifa ya Wahitimu wa Chuo Kikuu cha al Azhar mkoani Dakahlia ametilia mkwazo umuhimu wa Qur’ani Tukufu katika maisha ya kila mtu na nafasi yake katika kujenga pande mbalimbali za shakhsia ya kifikra na kivitendo ya mwanadamu akisema kuwa, Qur’ani Tukufu ina taathira kubwa sana katika kuijenga na kuiletea maendeleo jamii.