Jumuiya ya Haki za Wanadamu ya Kiislamu ya nchini Uingereza, imepanga kuitisha mkutano wake wa saba wa kila mwaka chini ya kaulimbiu ya kukabiliana na ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Ulaya.

Mtandao wa jumuiya hiyo umeripoti habari hiyo na kusema kwamba mkutano huo utafanyika kwa kushirikiana na Kanali ya Kimataifa ya Kukabiliana na Ukoloni (DIN). Mkutano huo wa saba wa kila mwaka wa jumuiya hiyo utafanyika kwa njia ya Inteneti na maudhui yake kuu itakuwa ni mashambulizi dhidi ya haki za kiraia, kibinadamu na kisiasa za Waislamu wa Ulaya.

Ripoti ya jumuiya hiyo imesema, mwaka 2011, serikali ya Uingereza ilipendekeza kutekelezwa siasa za kuzuia vijana kujiingiza kwenye aidiliojia za misimamo mikali hususan zile zinazodaiwa ni za Uislamu wa misimamo mikali. Mbinu inayotumiwa na serikali ya Uingereza ni kuwadhibiti vijana Waislamu maskulini, vyuo vikuu, misikitini na kupitia mifumo ya afya na kutumia nguvu za ukandamizaji kama vile kuwatia mbaroni, kuwasaili na kuwafunga jela vijana hao Waislamu.

Huko Ufaransa pia, rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron amependekeza mfumo wa kuwaorodhesha na kuwadhibiti vijana Waislamu kama ule uliokuwa unatumiwa na Hitler wa Ujerumani kuwadhibiti Mayahudi. Viongizi wa Waislamu nchini humo wamelazimishwa kutia saini tamko la pamoja la kusisitiza kwamba Uislamu ni dini, si mrengo wa kisiasa. Kila pale wazazi Waislamu wanapofungua mashtaka dhidi ya walimu waliowaonesha watoto wao vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW madarasani, wao ndio wanaitwa wahalifu na wanatishiwa kufukuzwa katika nchi hiyo. Aidha Ufaransa imepiga marufuku kusambazwa picha za uhalifu na ukandamizaji unaofanywa na jeshi la polisi na anayesambaza anahesabiwa ni mhalifu nchini humo.

Tovuti hiyo ya Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya Uingereza vile vile imeandika, huko nchini Austria pia, serikali ya nchi hiyo imepanga kupiga marufuku Uislamu wa kisiasa. Watu watakaokwenda kinyume na sheria hiyo hata kama wataachiliwa huru haraka jela, wataendelea kuwa chini ya uangalizi wa kielktroniki wa serikali ya nchi hiyo katika umri wao wote. Jumuiya na Misikiti itakayotiliwa shaka kujishughulisha na siasa, itafungwa na maimamu wa Misikti hiyo lazima wachujwe kwanza na wapate kibali cha serikali ya nchi hiyo.

Kiujumla haki za kiraia na kibinadamu za Waislamu zinakanyagwa na serikali za nchi mbalimbali za Ulaya, suala ambalo ni ishara ya wazi wa kuzuka tawala za kipolisi barani humo.

Mkutano huo wa saba wa Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya nchini Uingereza unatarajiwa kufanyika tarehe 13 mwezi huu wa Disemba. Maudhui zake nyingine zitakuwa ni pamoja na kujadili Uislamu wa kisiasa, maana na chanjaa zake mbalimbali. Suala la haki za kiraia na kibinadamu na kuongezeka vibaya ufashisti barani Ulaya ni maudhui nyingine itakayojadiliwa katika mkutano huo, kwa mujibu wa tovuti ya jumuiya hiyo.

(Visited 23 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!