Baraza Kuu la Waislamu wa Ujerumani na taasisi kadhaa za kijamii zimeanzisha muungano wa kupambana na chuki katika matabaka mbalimbali ya jamii ya Ujerumani. Baraza hilo limetoa mwito kwa taasisi hizo kushiriki katika harakati za taifa za kupambana na chuki na uadui dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Ujerumani.
Mtandao wa habari wa gazeti la El Khabar la nchini Algeria umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, harakati hizo zilianza jana Juni 24, 2021 chini ya kaulimbiu “Chuki hazina nafasi” na zitaendelea kwa muda wa siku 10. Harakati hizo zitamalizika katika siku ya kukumbuka mwaka alipouliwa kikatili mahakamani Ujerumani, Bi Marwa el Sherbini, mwanamke Muislamu mtunza vazi la staha Hijab raia wa Misri.
Muungano wa kupinga chuki unaoundwa na taasisi 47 za Kiislamu ndio muungano mkubwa zaidi wa kupambana na chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi dhidi ya Waislamu duniani.
Abdassamad el Yazadi, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Ujerumani amewaambia waandishi wa habari kuwa, vitendo vya chuki na mashambulizi ya kiuadui ni jambo la kila siku hivi sasa dhidi ya Waislamu na misiki nchini Ujerumani.
Amesema, takwimu zilizotolewa na serikali ya Ujerumani mwaka 2020 zinaonesha kuwa, mwaka huo kulisajiliwa kesi 950 za mashambulizi na vitendo vinavyotokana na chuki dhidi ya Waislamu katika nchi hiyo ya Ulaya Magharibi.
Ni vyema kukumbusha hapa kwamba Bi Marwa el Sherbini, alikuwa ni Muislamu mwenye asili ya Misri aliyekuwa akiishi nchini Ujerumani na mumewe na mtoto wao. Bibi huyo mchunga vazi la staha la Hijab alikuwa daktari wa kutengeneza dawa. Tarehe 1 Julai 2009 alipigwa visu na kuuliwa kikatili ndani ya mahakama na raia mmoja wa Ujerumani mwenye chuki za kidini. Bibi huyo aliuawa shahidi yeye na mwanawe wa miezi mitatu tumboni, akiwa na umri wa miaka 31 tu.