Viongozi wa eneo la Catalonia nchini Uihspania wameamua kuanzisha rasmi masomo ya dini tukufu ya Kiislamu katika skuli za serikali kuanzia mwaka huu wa wa masomo wa 2020-2021
Mtandao wa habari wa al Yaum al Sabi’i umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wakuu wa jimbo la Catalonia la Uhispania wamefikia uamuzi huo kutokana na kuongezeka sana idadi ya Waislamu jimboni humo.
Idara ya Elimu wa jimbo la Catalonia limepasisha mpango wa majaribio wa kusomeshwa dini tukufu ya Kiislamu katika shule za serikali kwenye mikoa ya Barcelona, Lleida, Girona na Tarragona katika mwaka wa masomo wa 2020-2021.
Viongozi wa jimbo la Catalonia wamelazimika kuanzisha masomo hayo kutokana na idadi ya Waislamu kuongezeka sana katika nchi hiyo ya Ulaya pamoja na maombi ya jamii za Waislamu na raia wengine wa Uhispania wanaowaunga mkono Waislamu.
Ikumbukwe kuwa jimbo la Catalonia lina Waislamu zaidi ya milioni mbili. Baada ya Catalonia, majimbo mengine yenye Waislamu wengi nchini Uhispania ni Andalusia na mji mkuu Madrid. Karibu nusu ya Waislamu wa Uhispania ni watu wa asili wa nchi hiyo na nusu nyingine ni wahajiri.
Viongozi wa Catalonia wamesema, mpango huo hivi sasa ni wa majaribio na iwapo walimu watapatikana na masomo kwenda vizuri, basi utatangazwa kuwa wa kudumu katika siku za usoni.