Misikiti nchini Uganda jana Ijumaa ilianza tena kutekeleza ibada za Sala ya Ijumaa baada ya kusimamishwa tangu mwezi Machi mwaka huu kutokana na janga la COVID-19.

Vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya Uganda vimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, katika hotuba zao, maimam wamewahimiza Waislamu kushikamana na dini yao, kulinda umoja na mshikamano na kutodharau fani mbalimbali za kielimu zenye maendeleo na za kuwapa ajira kwa kuchunga mafundisho ya dini yao.

Akihimiza suala hilo, Sheikh Burhan Ali, Imam wa Msikiti wa al Rahman wa mjini Kampala ametumia fursa za khutba za kwanza kabisa za Ijumaa tangu mwezi Machi, kuwahimiza Waislamu wajibidiishe kutafuta elimu za kila fani kwa manufaa yao, ya familia zao, ya jamii zao na ya dini yao.

Vile vile amewapongeza Waislamu waliofanikiwa kupata vyeti vya masomo muhimu ya juu na kushika nafasi mbalimbali serikalini na katika maeneo mengine, akiwataka watumie fursa hizo kuzisaidia vizuri jamii zao.

Katika sehemu nyingine ya khutba zake za Ijumaa, Sheikh Burhan Ali wa Msikiti wa al Rahman mjini Kampala Uganda amewaasa Waislamu waache mifarakano akisisitiza kwamba, kila Waislamu wanapozozana ndipo adui anapopata fursa ya kukandamiza haki zao. Serikali ya Uganda imeruhusu Waislamu wasiozidi 70 washiriki kwenye ibada za Sala ya Ijumaa. Masheikh nchini humo wametumia khutba za Ijumaa za jana kuiomba serikali iruhusu Waislamu zaidi washiriki kwenye ibada hiyo kwani misikiti inao uwezo wa kupokea idadi kubwa zaidi ya Waislamu na kuchunga vizuri masharti ya kiafya ya kujikinga na ugonjwa wa COVID-19.

(Visited 15 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!