Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya Monmouth na kusambazwa jana Jumatano, Novemba 18, 2020 yanaonesha kuwa, Wamarekani wamefurahishwa zaidi na kubwagwa na kupigwa na chini Donald Trump kuliko hata ushindi wa Joe Biden.

Mtandao wa habari wa The Hill wa nchini Marekani umeripoti kwamba, kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa karibuni kabisa wa maoni, karibu thuluthi nzima ya walioshiriki kwenye uchunguzi huo au tuseme asilimia 34 ya walioshiriki, wamesema kuwa wamefurahishwa zaidi na kushindwa Donald Trump huku asilimia 25 kati yao wakisema wamefurahishwa zaidi na ushindi wa Joe Biden.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni, asilimia 73 ya waliompigia kura Joe Biden wamesema wamefurahishwa zaidi na kuangushwa Donald Trump kabla ya hata kufurahisha ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa Novemba 3, 2020 wa rais wa Marekani suala ambalo linaonesha walipiga kura ya hasira ya kumchukia Donald Trump.

Matokeo ya uchunguzi huo aidha yanayonesha kuwa, asilimia 26 ya waliompigia kura Donald Trump wamesema wamekasirishwa na kushindwa mgombea wao huku asilimia 36 kati yao wakisema kwamba wamechukizwa na ushindi wa Joe Biden.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa, asilimia 38 ya wananchi wa Marekani wamekasirishwa na kushindwa Donald Trump katika uchaguzi huo wa Jumanne ya Novemba 3, 2020 huku asilimia 44 ya waliotoa maoni yao wakisema kuwa wamechukizwa na ushindi wa Biden.

Matokeo hayo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya Monmouth yanaonesha pia kuwa, asilimia 60 ya waliojibu maswali wamesema, ushindi wa Joe Biden ndio uadilifu na alistahiki kushinda, lakini asilimia 32 wamerudia madai ya Donald Trump kwamba Biden ameshinda katika uchaguzi uliochakachuliwa.

Uchunguzi huo wa maoni umewashirikisha watu wazima 810 raia wa Marekani na umefanyika baina ya tarehe 12 hadi 16 Novemba, 2020. Uwezekano wa kukosea matokeo ya uchunguzi huo ni wa asilimia 3.5.

(Visited 1 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!