Saa chache tu tangu baada ya kuapishwa kuwa rais wa 46 wa Marekani, Joseph Robinette Biden Jr. amekwenda katika Ikulu ya nchi hiyo White House na kutia saini amri na dikrii kadhaa za utekelezaji ikiwemo ya kufuta marufuku ya Donald Trump ya Waislamu kuingia Marekani.

Wakati wa kampeni za uchaguzi, Joe Biden aliahidi kwamba, katika siku ya kwanza kabisa ya urais wake, ataruhusu Waislamu kuingia Marekani na atafuta marufuku iliyowekwa na Trump. Vile vile aliwaahidi Waislamu kuwaingiza katika kila sekta ya utendaji ndani ya serikali yake. Kwa ahadi zake hizo bila ya shaka kura za Waislamu zilimsaidia kupata ushindi katika uchaguzi wa Novemba 3, 2020.

Mashirika ya habari ya Marekani yameripoti kwa wingi habari hiyo na kuongeza kuwa, katika siku ya kwanza ya urais wake, Biden ametia saini amri 17 za utekelezaji ikiwemo ya kufuta marufuku ya Trump kwa Waislamu kuingia nchini Marekani. Suala jingine ni kuirejesha Marekani katika Mkataba wa Hali ya Hewa wa Paris, kufanya kuwa jambo la lazima kutumia barakoa katika maeneo ya umma na kuondoa hali ya dharura iliyowekwa na Trump katika mpaka wa Marekani na Mexico. Hisia za kwanza kabisa rasmi kuhusu hatua hiyo ya Joe Biden zimeoneshwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ambaye amesema: “Nimeupokea kwa shauku uamuzi wa Rais Biden wa kuiunga tena Marekani katika mkataba wa Paris wa mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.”

(Visited 52 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!