Mahakama ya Umoja wa Ulaya (CJEU) imetoa hukumu ya kukandamiza uhuru wa mavazi wa wanawake wawili Waislamu wa nchini Ujerumani.

Vyombo mbalimbali vya habari kama France24, Reuters, Arabi21 n.k, vimeripoti habari hiyo na kusema kuwa, Mahakama ya Ulaya yenye makao yake Luxembourg imetoa hukumu ya kubariki na kuruhusu waajiri kuwafuta kazi wafanyakazi wao wanaovaa vazi la staha la Kiislamu, Hijab. 

Wanawake wawili Waislamu wa nchini Ujerumani walifungua kesi katika Mahakama ya Umoja wa Ulaya (CJEU) kulalamikia hatua ya waajiri wao ya kuwasimamisha kazi kwa sababu ya mavazi yao ya staha ya Hijab. Mmoja wa wanawake hao Waislamu alikuwa anafanya kazi katika kituo cha kulelea watoto wadogo, Chekechea na mwingine katika duka la bidhaa za nyumbani. 

Kwa mujibu wa hukumu hiyo ya mahakama ya CJEU, mwajiri anaweza kumsimamisha kazi mfanyakazi wake yoyote aliyevaa nembo yoyote ya kidini, kisiasa n.k, kwa kuzingatia mazingira yake ya kazi na hali ya wateja wake. Mara nyingi hukumu kama hizo hutolewa dhidi ya Waislamu lakini huongezewa baadhi ya maneno ili isionekane waliolengwa ni Waislamu.

Chuki dhidi ya Uislamu na kukabiliana na nembo za Kiislamu hasa vazi la staha la mwanamke Muislamu, Hijab, zimezua mjadala mkubwa barani Ulaya. 

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, hivi sasa kuna idadi kubwa ya Waislamu katika nchi za Ulaya na kwa mujibu wa sheria na katiba za nchi hizo, kila mtu yuko huru kufuata imani na itikadi anayopenda kama ambavyo kila mtu yuko huru katika kuchagua vazi analoona ni sahihi kwake. 

Pamoja na hayo, unyanyasaji wa wanawake Waislamu wanaovaa vazi la staha Hijab ni mkubwa sana katika nchi za Magharibi hasa barani Ulaya.

(Visited 100 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!