Kikao cha 12 cha kiuchumi baina ya Russia na nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC maarufu kwa jina la Baraza la Kazan, kimeanza katika makao makuu hayo ya Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, kikao hicho kimefunguliwa kwa Maonyesho ya Kimataifa ya Halal Expo. Zaidi ya watu 4000 kutoka kona mbalimbali za dunia wanashiriki kwenye kikao hicho. 

Rais Rustam Minnikhanov wa Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia ndiye aliyefungua maonyesho hayo ambapo katika sherehe za ufunguzi amesema,  nimezungumza na Waziri wa Ustawi wa Kiuchumi wa Russia, Maxim Reshetnikov kuhusu njia za kutanua wigo wa maonyesho hayo katika eneo pana zaidi la kijiografia kwa ajili ya kuvutia idadi kubwa zaidi inayowezekana na wawekezaji na washiriki.

Kazan, makao makuu ya Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia

Kwa upande wake, Waziri wa Ustawi wa Kiuchumi wa Russia, Maxim Reshetnikov amesema katika sherehe za ufunguzi wa maonyesho hayo kuwa, idadi ya Waislamu nchini Russia inafikia milioni 20. Idadi hiyo ni fursa nzuri sana kwa mashirika ya kimataifa yanayoshiriki kwenye maonyesho hayo. Aidha amewahakikishia washiriki kwamba makubaliano yoyote yatakayotiwa saini katika kikao na maonyesho hayo, yatasimamiwa na serikali yenyewe ya shirikisho la Russia ili kuhakikisha yanatekelezwa kivitendo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya shirika la habari la Anadolu, shabaha ya kuitishwa kikao hicho ni kuhamasisha ustawi wa taasisi za kifedha za Kiislamu nchini Russia, kutia nguvu uhusiano wa kibiashara, kiuchumi kielimu, kiufungundi, kijamii na kiutamaduni baina ya Russia na nchi za Kiislamu wanachama wa OIC. 

Kikao hicho cha “Baraza la Kazan 2021” kinamalizika kesho Ijumaa, tarehe 30 Julai, 2021.

(Visited 14 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!