Gazeti la The Economist la nchini Uingereza limeripoti kuwa, licha ya kwamba katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, Waislamu wamekuwa wakinyanyaswa, kukandamizwa na kushambuliwa kila upande lakini pamoja na hayo wameweza kuonesha nguvu zao, wamepata mafanikio muhimu ya kitaifa na idadi yao inazidi kuongezeka.
Gazeti la al Quds al Arabi limelinukuu gazeti hilo la kila wiki la The Economist linalochapishwa mjini London, Uingereza likiripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, licha ya kuweko unyanyasaji na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Marekani, lakini jambo hilo halikuwazuia kujiletea maendeleo na kupata mafanikio mauhimu ya kitaifa nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo miaka 20 iliyopita inaweza kuhesabiwa kuwa ni kipindi cha dhahabu kwa Waislamu wa Marekani kwani idadi yao imeongezeka na kufikia milioni 3.5 na nafasi yao katika jamii ya Marekani nayo inazidi kupanda.
Idadi ya Waislamu kuanzia mwaka 2001 na kuendelea imeongezeka maradufu huko Marekani. Idadi ya madaktari Waislamu katika jimbo la Michigan nchini Marekani imeongezeka kwa asilimia 15 licha ya kwamba idadi yao katika jimbo hilo ni asilimia tatu au chini ya asilimia tatu ya wakazi wote wa Michigan. Hiyo ni bila ya kuhesabu idadi nyingine kubwa ya wasanii, waandishi wa habari na wanasiasa Waislamu huko Marekani.
Gaeti la The Economist limeongeza kuwa, Mahershala Ali, Ayad Akhtar, Aziz Ansari na Hasan Minhaj, ni sehemu tu ya wacheza filamu na waandishi maarufu Waislamu waliofanikiwa kupata zawadi za kimataifa katika miaka ya hivi karibuni.
Rashida Tlaib na Ilhan Omar, ni wanawake wa kwanza Waislamu kufanikiwa kuingia bungeni nchini Marekani. Mbali na hao kuna idadi kubwa ya Waislamu ni wajumbe katika mabaraza ya shule na kwenye serikali za kieneo na mitaa huko Marekani.
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti hilo la The Economist la nchini Uingereza, baada ya kupita karne nne tangu Uislamu uingine nchini Marekani, hatimaye Waislamu wameweza kupata nafasi katika jamii ya nchi hiyo. Licha ya kwamba tangu mwaka 2001 mashambulizi dhidi ya Waislamu yameongezeka sana tena kila upande kwa shabaha ya kueneza chuki na uadui dhidi ya Waislamu hasa baada ya mashambulio ya Septemba 11, lakini idadi ya Waislamu inazidi kuwa kubwa huko Marekani.