Wizara ya Wakfu ya Misri imempa adhabu Imam mmoja wa msikiti nchini humo kwa madai ya kurefusha khutba za Ijumaa na kupindukia muda alioanishiwa.
Mtandao wa habari wa “al Misri al Yaum” umemnukuu Waziri wa Wakfu wa Misri, Mohamed Mokhtar Gomaa akisema kuwa, wizara hiyo imeamua kutompa Sheikh Amr al Sayyid, marupurupu ya miezi miwili ya mimbari kutokana na kutoa khutba mbili za Ijumaa kwa kupindukia muda aliopangiwa. Imam huyo wa ni msikiti mmoja wa mji wa Marsa Matruh ambao ndiyo makao makuu mkoa wa Matruh ulioko katika fukwe za Bahari ya Mediterranean nchini Misri.
Hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya idara ya wakfu ya mji wa Marsa Matruh na kupasishwa na mkuu wa kitengo cha masuala ya kidini cha Wizara ya Wakfu ya Misri. Wizara hiyo imesisitiza kuwa, sababu hasa ya kutolewa adhabu hiyo ni hatua ya Imam huyo kutoa hotuba kwa zaidi ya muda ulioainishwa na Wizara ya Wakfu ya Misri.
Ikumbukwe kuwa maimamu wa misikiti nchini Misri, mbali na kupangiwa hotuba wanazopasa kutoa, maudhui na maneno yake, wanapangiwa pia muda na dakika za kutoa hotuba hizo. Wizara ya Wakfu ya nchi hiyo imeweka sheria kali za kuhakikisha amri hiyo inatekelezwa kikamilifu.
Kwa mujibu wa sheria za Misri, maimamu hawatakiwi kupindukia dakika 15 katika khutba zao za Ijumaa. Wakati huu wa maambukizi ya corona, maimamu hao wamepunguziwa muda wa kutoa khutba hadi dakika 10 na anayepindukia muda huo anachukuliwa hatua.
Wizara ya Wakfu ya Misri imewataka waajiriwa wote wa wizara hiyo wachunge vizuri sheria na maelekezo ya watu wa afya ili kupunguza maambukizo ya COVID-19 kadiri inavyowezekana. Wizara hiyo imesema, haitosita kufunga msikiti wowote ule ambao wahusika wake hawatochunga protokali za kiafya za kupambana na ugonjwa wa corona.