Matatizo ya chakula yaliyojitokeza katika Chuo Kikuu cha Edinburgh huko Uskochi (Scotland) katika kipindi cha karantini ya COVID-19 na kulishwa sandwich za nyama ya nguruwe wanachuo Waislamu wa chuo hicho, kumezusha malalamiko makubwa ya kila upande.

Habari hiyo imeripotiwa na mashirika na magazeti mbalimbali ya habari kama The Sun la Uingereza, mtandao wa The Times n.k, na kuwanukuu wanafunzi Waislamu wa chuo cha Pollock Hall cha Chuo Kikuu cha Edinburgh wakisema kuwa, baada ya chuo kikuu hicho kuwekwa chini ya karantini na kufungwa maeneo yake ya chakula kutokana na wimbi la maambukizi ya kirusi cha corona, wanachuo Waislamu na wale wanaokula mbogamboga tu wasiokula nyama walilishwa nyama ya nguruwe na vyakula vingine ambavyo havina kiwango kinachotakiwa.

Mmoja wa wanachuo hao aliyejitambulisha kwa jina la Darcy Culverhouse amefichua kuwa, baada ya kuwekwa karantini kutokana na kirusi cha corona, wanachuo waliokuwa kwenye Diet na wanafunzi Waislamu walipewa chakula kisichofaa kabisa.

Mwanachuo huyo amehoji katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram kwamba vipi mwanachuo Muislamu ambaye hata nyama hali, analazimishwa kula sandwich zenye nyama ya nguruwe badala ya kupelekewa chakula halali kwake na kizuri kutoka nje ya majengo ya Chuo Kikuu?

Hivi sasa kuna maduka kadhaa ya eneo hilo ambayo yamepewa jukumu la kuwapa chakula na nyama wanafunzi Mayahudi kulingana na mafundisho ya dini yao, lakini inasikitisha kuona hilo halikuzingatiwa kwa wanachuo Waislamu. Chuo Kikuu cha Edinburg ni maarufu sana na kina historia ndefu huko Uskochi (Scotland). Chuo Kikuu hicho kiliasisiwa mwaka 1583 na ni katika vyuo vikuu vya daraja za juu duniani.

(Visited 31 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!