Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al Azhar cha nchini Misri leo Jumamosi kimeidhinisha kuanza masomo ya Qur’ani yaliyokuwa yamesimamishwa nchini humo kutokana na maambukizo ya kirusi cha corona.
Mtandao wa “Akhbarak” umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, harakati za vituo vya Qur’ani vya Misri ambazo zilikuwa zimesimamishwa kutokana na ugonjwa wa COVID-19 zitaanza tena baada ya Chuo Kikuu cha al Azhar kuidhinisha na kwa sharti la kuchungwa protokali zote za kiafya.
Miongoni mwa masharti ya kuanza tena masomo ya Qur’ani nchini Misri ni pamoja na kupiga dawa mtawalia kwenye madrasa na vituo vya Qur’ani, kuchunga masafa, kugawanywa wanafunzi katika vikundi vidogovidogo, kutengewa wakati maalumu kila kikundi na kulazimishwa kuvaa barakoa.
Vile vile Idara Kuu ya Masuala ya Qur’ani ya Misri imepewa jukumu la kusimamia vizuri na kwa karibu utekelezaji wa masuala yote hayo kwa kutuma wakaguzi mara kwa mara na kuchukua hatua za haraka za kisheria kwa watakaokwenda kinyume na masharti hayo.