Taasisi ya Mahusiano ya Mbari imetangaza habari ya kuanzishwa sheria mpya nchini Uingereza ambazo zinaruhusu kupokonywa uraia wa nchi hiyo Waislamu na kugeuzwa kuwa raia wa daraja la pili.

Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar imeinukuu Taasisi ya Mahusiano ya Mbari (Institute of Race Relations) ikitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa sera mpya za serikali ya Uingereza zinawageuza raia Waislamu wa nchi hiiyo kuwa wa daraja la pili. Hii ni kutokana na sheria zinazoruhusu Waislamu kupokonywa uraia wa Uingereza.

Kwa upande wake, gazeti la The Guardian la Uingereza nalo limeinukuu taasisi hiyo ikisema: Sheria ya Utaifa na Ulinzi wa Mipaka, ambayo inaruhusu kufutiwa uraia watu ambao wana uraia wa nchi nyingine, kimsingi inawalenga Waislamu. Sheria hiyo hiyo ya kibaguzi inaunda aina ya uraia ambayo ni duni kuliko Waingereza wengine.

Katika ripoti ya taasisi hiyo, imeelezwa kuwa sera za Uingereza zinawalenga zaidi Waingereza wa Asia Kusini, ambao wengi wao wanatoka katika jamii ya Waislamu.

Ripoti ya The Guardian pia imeeleza: Taasisi ya Mahusiano ya Mbari imechapisha ripoti hiyo baada ya utata uliojitokeza katika kadhia ya Shamima Begum. Msichana huyo mwenye umri wa miaka 15 ambaye alisafirishwa hadi maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Daesh (ISIS) huko Syria na Iraq, na kwa kuzingatia sheria iliyotajwa hapo juu, Uingereza ilimpokonya uraia wa Uingereza binti huyo.

Gazeti hilo limemnukuu Francis Weber, Naibu Mkuu Mtendaji wa taasisi hiyo na ambaye ndiye aliyechapisha ripoti hiyo akisema: “Ujumbe uliomo kwenye sheria ya uraia ya mwaka 2002 na utekelezaji wake, hasa dhidi ya Waislamu wa Uingereza wenye asili ya Asia Kusini, ni kwamba licha ya kuwa na hati za kusafiria za Uingereza, hawajawahi na hawatakuwa raia wa kweli wa nchi hiyo.

Weber anaongeza kuwa, wakati raia wa asili wa Uingereza anaweza kufanya uhalifu mbaya zaidi bila kuathiri uraia wake, hakuna hata raia takriban milioni sita wa Uingereza ambaye si raia asili wa nchi hiyo ana uhakika kuhusu kuendelea muda wote kubakia uraia wake wa Uingereza.

Amesema: Kabla ya sheria hiyo kuanza kutumika dhidi ya Abu Hamza al-Masri mwaka 2003, Uingereza ilikuwa haijawahi kufuta uraia wa raia yeyote katika kipindi cha miaka 30, lakini tangu kuanguka kukndi la Daesh nchini Syria mwaka 2017, London inachunguza kesi za watu 217 kwa lengo la kuwapokonya uraia wa Uingereza.

(Visited 36 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!