Joe Biden, mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Democrats ambaye ni mpinzani mkubwa wa rais wa hivi sasa wa Marekani, Donald Trump kwa mara nyingine ameahidi kuwashirikisha Waislamu katika sekta zote za uongozi iwapo atachaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo katika uchaguzi wa mwezi ujao wa Novemba, 2020.

Hayo yameripotiwa na Middle East Eye na kuongeza kuwa, kwa mara nyingine Joe Biden amerudia ahadi yake ya kufunguwa milango ya kuingia Waislamu nchini Marekani katika siku ya kwanza kabisa ya kushika hatamu za uongozi na kusisitiza kuwa, ataunda serikali itakayowashirikisha Wamarkeani wote wakiwemo raia Waislamu wa Marekani.

Biden ametuma ujumbe wa video kwa jumuiya ya Mawakili wa Waislamu na kusema kuwa, Marekani inahitajia umoja na mshikamano kukabiliana na chuki na taasubu zilizotanda kila sehemu nchini humo kutokana na uchochezi wa Donald Trump.

Amesema, imani ya wananchi leo hii inakaribia kutoweka kabisa. Badala ya Wamarekani kuwa na matumaini, sasa wameparaganyika nami sitoruhusu jambo hilo litokee. Tuna mustakbali unaong’ara sana na hatuwezi kuruhusu uzame kwenye chuki na vurugu.

Joe Biden alikuwa Makamu wa Rais wa Marekani wakati wa serikali ya Barack Obama. Amewaahidi Waislamu kwa kuwambia: Nikiwa Rais wa Marekani nitafanya juhudi zangu zote kuhakikisha sumu ya chuki inafutika katika jamii. Ninaheshimu mchango wenu. Serikali yangu itakuwa ya Marekani ambayo itawashirikisha Wamarekani Waislamu katika nyuga na daraja zote.

Baadhi ya uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa, Joe Biden amemshinda Donald Trump katika kura za maoni. Uchaguzi wa Rais wa Marekani unadarajiwa kufanyika tarehe 3 mwezi ujao wa Novemba, 2020.

(Visited 39 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!