Katika kipindi chote hiki cha kuenea janga la corona nchini Ujerumani, wananchi wa nchi hiyo wamekumbwa na woga, kukosa usalama na maswali mengi yasiyo na majibu. Uchunguzi unaonesha kuwa, Wajerumani wengi wamerejea kwa Mungu ili kupata utulivu, matumani na nguvu za kuendelea na maisha.
Hivi karibuni kuliitishwa kikao nchini Ujerumani kilichosimamiwa na taasisi ya Bertelsmann na kituo cha shirikisho la Ujerumani cha Mafunzo ya Kisiasa kilichopewa jina la “Imani Wakati wa Corona” na ndani yake wataalamu wa dini tofauti walizungumzia nafasi ya dini katika kutatua migogoro ya kijamii na kiutamaduni.
Wataalamu hao walisema kuwa, katika nyakati nzito kama kipindi cha mgogoro wa corona, imani ya Mwenyezi Mungu hupelekea watu kupata utulivu na huwa nguvu za kuendelea na maisha kupitia kuwa karibu kwao na Mwenyezi Mungu.
Bi Carole Hillenbrand mtafiti mashuhuri wa masuala ya Sayansi ya Jamii nchini Ujerumani na ambaye ni mmoja wa wataalamu wengi walioshiriki kwenye kikao hicho amesema kuwa, katika kipindi chote hiki cha janga la corona, wananchi wa Ujerumani wamekumbwa na woga, wasiwasi, kukosa amani na maswali chungu nzima yasiyo na majibu. Uchunguzi unaonesha kuwa, watu wengi nchini Ujerumani wanapata matumaini, utulivu na nguvu za kuendelea na maisha kila wanapomfikiria Mungu wakati huu mgumu wa corona. Katika hotuba yake hiyo, Bi Hillenbrand amegusia uchunguzi uliofanyika nchini Ujerumani na kusema, kwa mujibu wa uchunguzi huo ambao matokeo yake yalitangazwa mwezi Mei mwaka huu wa 2021, asilimia 32 ya Wajerumani walioshiriki kujibu maswali walisisitiza kuwa, imani yao kwa Mungu na kupenda kutekeleza mafundisho ya dini imeongezeka sana wakati huu wa corona.
Mtafiti huo aligusia pia imani za kiroho zilizobuniwa na wanadamu na kusema kuwa, imani za kimaanawi na kiroho zisizo za kidini zilizobuniwa na wanadamu, nazo zimepata wafuasi. Hata hivyo kwa vile imani hizo zilizotengenezwa na wanadamu hazina misingi sahihi, huwa zinapoteza umaarufu wake baada ya muda mfupi.
Bi Carole anaendelea kusema: “Ninaamini kwamba dini za Mwenyezi Mungu ndiyo marejeo pekee ya maisha ya mwanadamu. Mijadala na mazungumzo ya kiutaalamu baina ya wafuasi wa dini mbalimbali za Mwenyezi Mungu ni jambo la lazima. Kwa kweli katika jamii ya watu ambao ni wa dini tofauti, wenyewe watu hao wanaujua vyema wajibu wa kuwa na mazungumzo baina yao ili waweze kuishi kwa kuheshimiana na kuendelea vizuri na maisha yao.”