Kitendo cha kutumia emoji za WhatsApp kwa sura ya kuwafanyia istihzai watu wengine kinaweza kumfungisha jela mtu kwa miaka isiyopungua mitatu au faini isiyopungua Riali 5,000 za Oman.
Hayo yamebainishwa na Mwanasheria Salah Ali Meqbali katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na gazeti la kila siku la Times of Oman kuhusu kuwatumia raia wa Oman na wasio wa Oman, emoji na vibonzo vya istihzai na visivyostahiki kupitia WhatsApp. Ameongeza kuwa, katika siku za hivi karibuni, emoji za Oman na zisizo za Oman zimeenea katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp kuwalenga raia wa Oman na wasio wa Oman tena kwa sura isiyostahiki na ya kufanya istihzai.
Mwanasheria Meqbali aidha amesema: Kutengeneza na kutuma kupitia WhatsApp, emoji za picha za watu na kuwaonesha kwa sura ya kuwadhalilisha na kuwafanyia istihzai bila ya ridhaa yao, kunahesabiwa ni uvunjaji wa haki na mipaka ya maisha binafsi ya watu.
Aidha amesistiza kuwa kitendo hicho ni kosa kwa mujibu wa sheria za Oman na kinaweza kupelekea mtendaji wa kosa hilo kufungwa jela kwa muda usiopungua mwaka mmoja na usiopindukia miaka mitatu, pamoja na faini isiyopungua Riali 1,000 na isiyopindukia Riali 5,000 za Oman (takriban dola 13,000 za Marekani) au moja ya adhabu hizo mbili.