Na Mohammed K. Ghassani
******
Wajipigao vifua, kwa kujiita washindi
Ilhali wanajuwa, visa na vyao vitimbi
Hawepewa wechukua, kwa nguvu, kyedi na shindi
Wakae wakitambuwa, hivyo safari hayendi.
*******
Wajisifuo amani, weilinda kwa weledi
Hali wajuwa yakini, risasi na mijeledi
Ilitua miilini, na kutoboa fuadi
Nawalilia Yamini, katu safari hayendi
*******
Watajao kususana, na vituko vya vipindi
Wasitaje kuuwana, raundi hadi raundi
Huwa kama watuona, hatu watu, tu mabundi
Hawa nawapa bayana, safari hivyo hayendi
*******
Watakao tusamehe, ela radhi hawaombi
Bali wa kwenye sherehe, kuwatukuza mazombi
Kutugeuza mapenhe, tusiojua ulumbi
Hata waite Mashekhe, huwa safari hayendi
*******
Toba huitwa nasuha, ikayafuta madhambi
Paombwapo msamaha, kwa twaa si ujigambi
Msiba huwa furaha, adui hupewa shambi
lakini penye karaha, juwa safari hayendi
Bonn
20 Disemba 2020