Serikali ya Jakarta imejiwekea malengo ya kuigeuza Indonesia kuwa kituo kikuu cha bidhaa halali duniani ifikapo mwaka 2024.

Mtandao wa habari wa Antara News wa nchini Indonesia umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, ijapokuwa hivi sasa nchi za Brazil, Australia, Japan, nchi za Amerika ya Kaskazini na China ndio wazalishaji wakuu wa bidhaa halali, lakini wataalamu na viongozi wa Indonesia wanasema kuwa, nchi yao ambayo ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu duniani na ni ya nne kwa kuwa na watu wengi zaidi ulimwenguni, inapaswa kutumia vizuri fursa na nguvu zake hizo na kuwa kituo kikuu cha uzalishaji wa bidhaa halali.

Makamu wa Rais wa Indonesia, Ma’ruf Amin

Makamu wa Rais wa Indonesia, Ma’ruf Amin hivi karibuni alizungumzia data na takwimu za kimataifa za uchumi wa Kiislamu za mwaka 2019 na kusema kuwa, mwaka huo bidhaa za halali zilizosafirishwa nje ya Brazil zilikuwa na thamani ya dola bilioni 5.5 huku Australia ikinufaika na uzalishaji wa bidhaa halali mwaka huo kwa kukusanya dola bilioni 2.4 za mauzo ya bidhaa hizo.

Makamu huyo wa rais wa Indonesia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu wa masuala ya sheria za uchumi wa Kiislamu. Amesema, lengo lake ni kuigeuza Indonesia kuwa kituo kikuu cha kuzalisha bidhaa halali duniani ifikapo mwaka 2024.

Ameashiria pia wajibu wa nchi za Waislamu kutumia vizuri fursa hiyo na kusema kwamba tunapaswa kuongeza kiwango cha uzalishaji wa bidhaa halali nchini Indonesia kwani sasa hivi nafasi ya bidhaa za nchi hiyo katika soko la bidhaa halali duniani ni asilimia 3.8 tu.

Itakumbukwa kuwa, bidhaa za halali zina soko kubwa duniani. Mwaka 2018, mahitaji ya bidhaa hizo duniani yalikuwa na thamani ya dola trilioni 2.2 za Kimarekani na inatabiriwa kwamba ifikapo mwaka 2024 mahitaji ya bidhaa za halali yatafikia dola trilioni 3.2 kote ulimwenguni.

(Visited 43 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!