Kiongozi Mkuu wa kidini wa Iran ametuma ujumbe wa maandishi na kulaani kitendo cha jarida la Charlie Hebdo la Ufaransa cha kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.
Katika ujumbe wake huo, Ayatullah Ali Khamenei amesema, dhambi kubwa na isiyosameheka ya jarida hilo la Ufaransa ya kumvunjia heshima Mtume Mtukufu, Nabii wa nuru na rehema SAW kwa mara nyingine imedhihirisha jinsi taasisi za kisiasa na kiutamaduni za ulimwengu wa Magharibi zilivyo na chuki na uadui na Uislamu na jamii nzima ya Waislamu.
Amesema, hatua ya viongozi wa Ufaransa ya kuinyamazia kimya dhambi hiyo kubwa kwa kisingizio cha kuweko uhuru wa kubainisha mambo; yenyewe ni uhalifu mkubwa, haukubaliki na ni kujaribu kudanganya watu.
Kiongozi Mkuu wa kidini wa Iran aidha amesema, siasa za Kizayuni za tawala za kibeberu ndiyo sababu hasa ya kuweko vitendo vya kihalifu vya maadui wa Uislamu huko Magharibi. Amesema, lengo la kuzushwa wimbi jipya la kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu sasa hivi (kama kuvunjiwa heshima Mtume huko Ufaransa na kuchomwa moto nakala ya Qur’ani Tukufu nchini Sweden) ni kupotosha fikra za walimwengu zisishushulishwe na njama chafu za Marekani na Israel katika ulimwengu wa Kiislamu.
Aidha ametoa mwito kwa mataifa ya Waislamu hasa hasa nchi za Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) kuzidi kuwa macho mbele ya masuala ya ulimwengu wa Kiislamu na wasinyamazie kimya wala kusahau uadui wanaofanyiwa Waislamu popote pale duniani.
Jumanne iliyopita, jarida la Charlie Hebdo la Ufaransa lilifanya utovu wa adabu wa kuchapisha kibonzo kinachomvunjia heshima Nabii wa rehma, Mtume Muhammad SAW, jinai ambayo imewakasirisha Waislamu wa ulimwengu mzima na kila mwenye fikra huru duniani.