Mtandao wa Utafiti wa Waislamu wa Uingereza (MBRN) una nia ya kuitisha kongamano mwezi Disemba mwaka huu kuhusu athari za COVID-19 kwa Waisamu wa nchi hiyo.

Taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya mtandao huo imesema kuwa, kongamano hilo litafanyika kwa njia ya Intaneti chini ya kaulimbiu “Waislamu wa Uingereza na COVID-19; Athari, Uzoefu na Radiamali.”

Miongoni mwa ajenda za kongamano hilo ni pamoja na: Athari za COVID-19 kwa Waislamu ikilinganishwa na watu wa dini nyinginezo nchini Uingereza, mchango wa dini ya Kiislamu katika kukabiliana na ugonjwa huo. Nafasi ya taasisi za misaada na za kujitolea za Waislamu katika kukabiliana na athari mbaya za kirusi cha corona, mchango wa maulamaa na viongozi wa Kiislamu, athari za corona katika familia za Waislamu na jinsi vyombo vya habari vinavyowaangalia Waislamu katika masuala yanayohusiana na ugonjwa wa COVID-19.

Waislamu nchini Uingereza wanachukua hatua zinazotakiwa kujikinga na corona

Tarehe ya mwisho ya kuwasilisha makala za washiriki wa kongamano hilo ni tarehe 30 mwezi huu wa Oktoba.

Uchunguzi unaonesha kuwa, tabaka lililoathiriwa zaidi na ugonjwa wa corona nchini Uingereza ni jamii za watu wachache kama Waingereza wenye asili ya Afrika na wenye asili ya Asia. Hata hivyo kiwango cha athari hizo kati ya jamii ya wachache ya Waislamu nchini humo hakijajulikana vyema.

Hadi leo mchana, Jumamosi, Oktoba 17, 2020, idadi ya wagonjwa wa COVID-19 waliotangazwa na serikali ya Uingereza walikuwa ni 689,257. Kati ya hao, 43,429 walikuwa wameshafariki dunia.

(Visited 20 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!