Sheikh Mkuu wa Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri maarufu kwa jina la Shaikhul Azhar, ametuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook na kusema kuwa, kitendo cha maadui wa Uislamu cha kuchoma moto nakala ya Qur’ani Tukufu nchini  Sweden ni jinai, ugaidi na uhayawani.

Televisheni ya al Alam imeripoti habari hiyo kwenye mtandao wake wa habari za lugha ya Kiarabu na kuongeza kuwa, Mufti wa al Azhar, (Shaikh al Azhar) Dk Ahmad al Tayyib amesema watu waliojipa uthubutu wa kufanya jinai ya kuchoma moto nakala ya Qur’ani huko nchini Sweden wanapaswa kutambua kuwa, jinai kama hizo ni unyama, uhayawani na ni ugaidi katika sura zake zote.

Amesema, jinai hiyo ni kitendo cha kibaguzi na kinachochukiza ambacho kinapingwa na kila ustaarabu wa mwanadamu aidha kinachochea vitendo vya kigaidi ambavyo vinaitesa dunia sasa hivi, mashariki na magharibi yake.

Shaikhul Azhar ameongeza kuwa, ni jambo lisilo na shaka kwamba kitendo hicho cha kiuadui kinachochea moto wa chuki, kinahatarisha usalama wa jamii za wanadamu na kinatishia kupotea matumaini yaliyopatikana hadi sasa katika mazungumzo baina ya dini na tamaduni mbalimbali.

Vile vile amesema, waliochoma moto nakala ya Qur’ani Tukufu huko Sweden wanapaswa kutambua kuwa, kitendo hicho kiovu kimejeruhi hisia za karibu Waislamu bilioni moja duniani na historia tayari imerekodi kitendo hicho cha kinyama, kijinai na cha aibu. Itakumbukwa kuwa Ijumaa iliyopita ya tarehe 28 Agosti 2020, maadui watatu wa Uislamu kutoka Denmark walichoma nakala ya Qur’ani Tukufu katika eneo la Rosengård, mjini Malmö, kusini mwa Sweden, jinai ambayo imewakasirisha mno Waislamu karibu bilioni moja katika kona zote za dunia.

(Visited 8 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!