Kuwait imeazimia kujenga Makumbusho makubwa zaidi duniani kuhusu maisha na sira ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kumnukuu Fehaid al Deehani, Mkurugenzi Mkuu wa wa Jopo la Umma la Kusimamia Uchapishaji na Usambazaji wa Qur’ani Tukufu na Sira ya Mtume la Kuwait akisema hayo katika mahojiano na gazeti la al Ambaa la Kuwait na kuongeza kuwa, nchi hiyo karibuni hivi itakuwa mwenyeji wa Makumbusho makubwa zaidi duniani kuhusu maisha ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Eneo hilo litakuwa na ukubwa wa mita mraba 25,000.

Amesema, Makumbusho hayo yatajumuisha kumbi 14 zitakazokuwa na maonyesho mbalimbali kuhusu maisha ya Bwana Mtume SAW kwa lugha zote hai duniani. Zitakuweko pia nakala za kale zilizoandikwa kwa mkono na zilizo nadra sana za Qur’ani Tukufu.

 Ameongeza kuwa, wananchi wa Kuwait na wasio wa Kuwait, kutoka mataifa na dini yoyote ile wataweza kutembelea Makumbusho hayo ili kupata kwa karibu na japo kidogo picha ya maisha yaliyojaa rehema ya mwanadamu bora kabisa duniani, ambaye ametumwa na Mwenyezi Mungu kuwa rehema kwa wanadamu wote. Jopo la Kusimamisha Uchapishaji na Usambazaji wa Qur’ani Tukufu la Kuwait litafanya juhudi za kuhakikisha kuwa, mradi huo mkubwa unafanikishwa kwa njia bora kabisa na kulingana na hadhi ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

Hata hivyo al Deehani hakusema ni wakati gani na muda utakaotumiwa kufanikisha mradi huo mkubwa. Hata Wizara ya Wakfu ya Kuwait nayo hadi hivi sasa haijatoa tamko lolote kuhusu mradi huo ambao pamoja na mambo mengine, unalenga kuhamasisha na kukuza utalii wa kidini nchini humo.

(Visited 77 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!