Wizara ya Wakfu ya Misri imeitisha mashindano ya kwanza kabisa ya aina yake kwa lengo la kuimarisha uzingatiaji wa malengo, maana na shabaha za Qur’ani Tukufu. Mashindano hayo yatahusisha watu wa rika na umri tofauti nchini humo.

Mtandao wa el Nabaa wa Misri umeripoti habari hiyo na kuinukuu Wizara ya Wakfu ya Misri ikitangaza kuwa, mashindano hayo yatahusiana na welewa jumla wa sura za Qur’ani Tukufu. Lengo lake ni kutia nguvu tadibiri na kutambua malengo na shabaha za aya za Qur’ani Tukufu na kuachana na kukisoma kijuu juu tu kitabu hicho kitakatifu.

Makundi mbalimbali ya rika na umri tofuati yatachuana kwenye mashindano hayo. Kwa mujibu wa ratiba, watoto wa chini ya miaka 12 watashindana katika kuelewa sura za juzuu ya 30 ya Amma na Surat Maryam. Vijana wa chini ya miaka 18 watashindana katika kuelewa malengo jumla ya sura za juzuu ya 28 na Surat Yusuf. Wahadhiri, watoaji mawaidha na walimu watachuana katika visa vya Mitume ndani ya Qur’ani Tukufu na surat al Kahf. Maimamu wa sala za jamaa na baadhi ya walimu watachuana katika uchambuzi wa mifano iliyomo kwenye aya za Qur’ani Tukufu na sura za al Aaraf, al Anfal, al Tawbah, Yunus na Hud.

Washindi wa mashindano hayo wameahidiwa kupewa zawadi nono na Wizara ya Wakfu ya Misri. Watakaoshinda kati ya watoaji mawaidha na maimamu wa sala za jamaa na walimu, watapewa ajira katika wizara hiyo ya wakfu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Wakfu ya Misri, wanaoshiriki kwenye mashindano hayo walianza kujiandikisha jana Jumapili, Agosti 23, 2020 na uandikishaji huo utaendelea kwa muda wa wiki moja.

(Visited 59 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!