Katika juhudi za kustawisha na kuongeza pato linalotokana na utalii wa kidini na wa Kiislamu, serikali ya Brunei imeamua kuitisha warsha na semina mbalimbali za kuongeza welewa wa wananchi wake kuhusu vivutio vya kidini nchini humo.
Kwa mujibu wa tofauti ya Borneo Bulletin, hivi sasa karibu watu 30 wameshiriki kwenye semina iliyoandaliwa na taasisi ya kustawisha utalii ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya nchi hiyo (MPRT). Lengo la warsha hiyo ni kuongeza welewa wa wananchi wa Brunei kuhusu misingi ya utalii wa kidini wa Kiislamu na vivutio vyake nchini humo.
Semina hiyo ni ya siku tatu na ilianza Jumanne, Mei 25, 2021 na inamalizika leo Alkhamisi, Mei 27, 2021. Miongoni mwa mafunzo yaliyotolewa kwenye warsha hiyo ni miongozo kwa asasi zenye vibali vya kuongoza watalii na kupewa elimu zaidi kuhusu masuala muhimu ya utalii wa kidini na wa Kiislamu.
Warsha hiyo ni sehemu ya mikakati ya serikali ya Brunei ya kuimarisha sekta ya utalii na kukuza vivutio vya sekta hiyo muhimu inayoiingizia Brunei pato kubwa kutoka ndani na nje ya nchi hiyo.
Brunei ni nchi ya kusini mashariki mwa Asia. Uchumi wa nchi hiyo ya kifalme unategemea usafirishaji nje bidhaa, mafuta, mbao, mpira na gesi asilia.
Miaka ya hivi karibuni, soko la mafuta limeharabika duniani hivyo serikali ya Brunei imejipanga kuongeza pato lake kupitia utalii wa kidini wa Kiislamu na umewekeza sana katika sekta hiyo. Karibu wananchi wote wa Brunei, ni Waislamu.