Mbunge mmoja nchini Mauritania ameitaka serikali ya nchi hiyo kutumia vizuri fursa ya usomeshaji Qur’ani ili kujenga jamii salama, tiifu na iliyopambika kwa sifa bora za kibinadamu na kimaadili.
Mbunge Ould al Khalifa aidha ameitaka serikali ya nchi hiyo ilipe umuhimu mkubwa suala la kusomesha na kuhifadhisha watoto Qur’ani kuanzia chekechea kwani jambo hilo litasaidia sana kuwa na jamii ya watu wema itakayopunguza uhalifu katika jamii na itakayopelekea kutawala mazingira bora ya kimapenzi na kiroho katika jamii.
Katika kikao cha bunge kilichojadili ilani ya serikali ya Waziri Mkuu Mohamed Ould Bilal, mbunge huyo amesema, bunge la Mauritania linaunga mkono kusomeshwa Qur’ani katika vituo vyote vya elimu vya nchi hiyo. Amesisitiza kuwa, malezi ya kiQur’ani ya taifa na jamii yoyote ile huwaongoza watoto wa taifa hilo kwenye njia nzuri, huleta utulivu katika jamii, usawa, uadilifu, mapenzi, ushirikiano, kuhurumiana na watu wote katika jamii hiyo kuishi kwa kusaidiana.
Mbunge huyo wa Mauritania pia ameitaka serikali ya nchi hiyo kuanzisha kampeni ya usomeshaji Qur’ani kwa njia ya Intaneti na kuziunganisha shule na chekechea zote katika mfumo wa masomo ya Intaneti hasa wakati huu wa kipindi cha corona. Amesema, matunda ya kampeni kama hiyo ni kuziletea ustawi wa haraka nchi ndogo za Afrika iwapo zitatumia Intaneti katika sekta zao zote hasa za kiuchumi.
Mbunge Ould al Khalifa amegusia pia umuhimu wa kuweko vituo vikubwa vya kuharakisha ustawi katika maeneo tofauti ya nchi hiyo akisisitiza kuwa, kuwasaidia wazalishaji wa ndani hasa wakulima, wavuvi, watu wa madini na wafugaji kutawapa ajira watu hasa vijana na kuwafanya wabakie katika maeneo yao na wasikimbilie kuzurura kwenye miji mikubwa.