Mkuu wa Masuala ya Msikiti Mtukufu wa Makkah (Masjid al Haram) na Msikiti wa Mtume huko Madina (Masjid al Nabi) nchini Saudi Arabia ametangaza kuanza mpango wa kuwashirikisha wanawake katika utoaji huduma kwenye Misikiti hiyo miwili mitakatifu.
Shirika la habari la Sputnik limetangaza habari hiyo na kusema kuwa mpango huo ulianza rasmi siku chache zilizopita sambamba na maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Ulimwenguni.
Abdul Rahman Ibn Abdul Aziz al Sudais, Mkuu wa Masuala ya Masjid al Haram na Masjid al Nabi amesema, kuweko wanawake katika timu ya kutoa huduma katika Misikiti hiyo ni jambo muhuimu sana hivyo uongozi wa maaeneo hayo matakatifu umeanzisha masomo maalumu ya kuainisha wanawake waliotimiza sifa za kusimamia huduma katika Misikiti hiyo.
Amesema, kupitia mpango huo wanafunzi watapata utaalamu na maarifa ya kiufundi ya usimamiaji na utoaji huduma ili wawe na uwezo wa kupanga ratiba maalumu za kutoa huduma katika maeneo hayo mawili matakatifu.
Sheikh Sudais pia amesema, mpango huo unatarajiwa kuongeza nafasi za wanawake katika usimamiaji na uendeshaji wa masuala ya Misikiti hiyo miwili mitakatifu na anataji kwamba, mikakati ya Saudia itatekelezeka vizuri na huduma katika Misikiti hiyo mitakatifu zitatolewa kwa njia bora zaidi.