Msanii mmoja raia wa Pakistan amepata taufiki ya kufuma aya zote za Qur’ani Tukufu kwenye penseli 8,000 katika kipindi cha miaka 10.

Tovuti ya lugha ya Kiarabu ya televisheni ya al Jazeera imeripoti habari hiyo na kumtaja msanii huyo kwa jina la Shahnawaz Malhi ambaye ni afisa mstaafu wa jeshi la polisi la Pakistan. Msanii huyo amefanikiwa kufuma sura zote 114 za Qur’ani Tukufu kwa kutumia nyuzi juu ya penseli 8,000.

Idadi ya penseli zilizotumika katika kila sura moja zimetemea urefu wa sura yenyewe, baadhi ya wakati ni penseli 50 hadi 70 na baadhi ya wakati ni penseli 100 hadi 500.

Penseli zote hizo amezitundika kwenye ubao kwa kutumia vifungo maalumu vya plastiki na kila sura ameiweka kwenye fungu lake maalumu na ubao wenyewe umenakshiwa maumbile ya Mwenyezi Mungu kama sayari na kutoa mvuto wa kipekee.

Akizungumzia jitihada yake hiyo, msanii huyo Mpakistan anasema, mwaka 2014 alistaafu katika jeshi la polisi kwenye jimbo la Sindh la Pakistan. “Mimi ni msanii wa kwanza kupata taufiki ya kufuma aya zote za Qur’ani Tukufu juu ya penseli,” amesema.

Anasema, alipenda kazi ya usanii akiwa bado mdogo, wakati akiwa bado shule ya msingi. “Nimeishi na ndoto yangu hiyo hadi mwaka 2002 nilipopata taufiki ya kuandika majina matakatifu ya Allah kwa hati za Kiarabu na kuyaonesha katika maonesho ya sanaa ya mji wa Karachi, Pakistan,” ameendelea kusema msanii huyo raia wa Pakistan.

Shahnawaz Malhi anasema, nimefanya kazi nzito kwa muda wa miaka 10, kila siku masaa 8 hadi nimefanikiwa kufuma aya zote za Qur’ani Tukufu juu ya penseli. Ili kuifanikisha kazi hii muhimu, nimepata msaada kutoka kwa familia yangu na marafiki zangu wenye thamani ya rupia milioni 3 (sawa na dola 16,760 za Kimarekani).

Hapa chini tumeweka baadhi ya picha za kazi muhimu sana za msanii huyo raia wa Pakistan.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!