Msikiti mmoja wa kihistoria wa mjini Durban Afrika Kusini umeteketea kwa moto jana Jumatatu Agosti 24, 2020 na maafisa wa Zima Moto wameshindwa kufanya chochote.
Mtandao wa “Akhbar 24” umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa Msikiti wa kihistoria wa Sala ya Ijumaa wa mjini Durban Afrika Kusini umeteketea kwa moto, na juhudi za maafisa wa zima moto zimeshindwa kuzuia msikiti huo usiteketee kwa moto.
Robert Makenzi, msemaji wa Zima Moto mjini Durban amesema, moto huo umesababisha hasara pia kwenye majengo matatu jirani na msikiti huo na kwamba maafisa wa zima moto walishindwa kuzima moto huo katika juhudi zao za masaa mawili.
Hata hivyo amesema, moto huo haukufika kwenye eneo la chini la msikiti huo wala hakuna mtu aliyejeruhiwa kwani wahudumu wote wa msikiti huo waliwahi kutoka nje.
Kwa upande wake, Sheikh Faisal Suleiman, Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Afrika Kusini amesema, inavyoonekana moto huo ni ajali tu imetokea na wala si jinai na huenda umetokana na hitilafu za umeme katika moja ya nyuma za wafanyakazi ndani ya msikiti huo. Msikiti huo wa Ijumaa wa mjini Durban Afrika Kusini umejengwa zaidi ya miaka 139 iliyopita na ni moja ya misikiti mikubwa nchini Afrika Kusini. Msikiti huo ulikuwa na uwezo wa kupokea karibu Waislamu elfu saba kwa Sala ya jamaa kwa wakati mmoja. Watu mbalimbali mashuhuri kama Nelson Mandela, Muhammed Ali (mwana masumbwi maarufu wa Marekani) na Yusuf Islam msoma kasida maarufu wa Uingereza, wamewahi kutembelea msikiti huo.