Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu (CAIR) katika jimbo la California limetangaza habari ya kuteuliwa mubalighi wa Kiislamu wa kwanza kabisa kuwa mwakilishi katika bunge la jimbo hilo.

Anthony Rendon, mkuu wa baraza hilo katika jimbo la California alisema jana Jumatatu, Disemba 7, 2020 kwamba Imam Mohammad “Yasir” Khan (pichani hapa chini), ameteuliwa kuwa Sheikh wa Bunge la Jimbo la California kwa mwaka 2021-2022.

Imam Yasir Khan

Hii ni mara ya kwanza kwa mubalighi wa Kiislamu kuingia katika bunge hilo bali kuwahi kuingia katika bunge lolote la jimbo nchini Marekani. Sheikh Yasir Khan atakuwa anafungua vikao vya bunge hilo kwa dua.

Basim Elkarra, mkurugenzi mtendaji wa baraza la CAIR huko California amesema, tunamshukuru spika wa bunge la California kwa uteuzi wake huu wa kihistoria na kwa kutekeleza ahadi zake za kuwa na California ya sura za kila namna inayowashirikisha watu wote. Maelfu ya wananchi wa California wamenufaika na huduma za kijamii za Sheikh Yasir Khan kwa miaka mingi, na bila ya shaka yoyote watafurahi na kufarijika sana kumuona Sheikh Yasir yumo katika bunge la jimbo hilo.

Kwa upande wake, Sheikh Yasir Khan amesema, ni fakhari kwangu kuona nimeteuliwa kuwa mjumbe wa Bunge la California nikiwa kiongozi wa dini na nitatumikia nafasi hiyo kwa udhati wa moyo wangu. Kitu kilichoifanya California kuwa na hadhi ni sisi kuweza kukubaliana na mitazamo tofauti katika kujenga madaraja ya pamoja ya kutuvusha salama na kutufikisha kwenye mustakbali bora.

Imam Yasir Khan ni mkuu wa Baraza la Taasisi za Kiislamu za Sacramento Valley (COSVIO). Vile vile ni muasisi wa taasisi ya NGO ya al Misbah ambayo inawasaidia wakimbizi na familia zao kifedha na kwa misaada isiyo ya kifedha. Vile vile ni Sheikh anayetoa mawaidha kwa wafungwa wa jela ya Kaunti ya San Joaquin na kwa wagonjwa wa hospitali ya Lodi Memorial.

Imam Yasir Khan amezaliwa na kukulia huko huko Sacramento. Masomo yake ya chuo kikuu ameyasomea katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Afrika Kusini.

(Visited 63 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!