Wizara ya Elimu ya Uturuki imetangaza kuwa, mwalimu mkuu na mwalimu wa darasa la nne mkoani İzmir nchini humo wamesimamishwa kazi kwa kumzuia mtoto aliyevaa vazi la staha la Hijab, kuingia darasani.

Shirika rasmi la habari la serikali ya Uturuki la TR limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Wizara ya Elimu ya nchi hiyo imeanzisha uchunguzi kuhusu taarifa kwamba mkuu wa skuli moja ya msingi na mwalimu mmoja wa kike walimzuia mtoto wa kike mwenye Hijab kuingia darasani katika skuli hiyo iliyoko kwenye wilaya ya Bayrakli mkoani İzmir, magharibi mw Uturuki.

Wakati mwalimu huyo wa kike wa darasa la nne alipokataa kumpokea msichana wa miaka 11 kwa sababu ya kuvaa vazi la staha la Hijab, mwama wa binti huyo alikwenda kuishitaki skuli hiyo.

Kufuatia hatua hiyo, Wizara ya Elimu ya Uturuki ilianza kufanya uchunguzi mara moja kuhusu tukio hilo na kutoa tamko ikisema, imemsimamisha kazi mwalimu mkuu na mwalimu huyo wa darasa la nne kutokana na kumnyima mtoto huyo haki yake ya kupata elimu.

Tamko la Wizara ya Elimu ya Uturuki limesisitiza kuwa, kumnyima mtu yoyote kupata elimu kwa sababu ya kuvaa vazi la Kiislamu ni jambo lisilokubalika na uchunguzi wa kina unaendelea kuhusu tukio hilo. Mwezi Februari mwaka huu pia, Mahakama ya 60 ya awali ya rufaa ya mjini Istanbul Uturuki ilimuhukumu mwanamke mmoja kifungo cha mwaka mmoja na miezi minne jela baada ya kumpata na hatia ya kuwashambulia wasichana wawili wenye Hijab katika eneo la Karakoy mjini Istanbul. Mwanamke huyo alihukumiwa kifungo hicho jela kwa kupatikana na hatia ya kuwadhalalilisha na kuwanyanyasa raia wawili wa Uturuki kutokana na chuki zake za kibaguzi.

(Visited 91 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!