Polisi nchini Sweden wamekandamiza maandamano ya watu wanaopinga kuchomwa moto Msahafu. Polisi hao wamekandamiza maandamano hayo na kumtia nguvu mmoja wa waandamanaji baada ya kusikika akipiga takbiri na kusema Allahu Akbar. Maandamano hayo yamefanyika kwenye mji wa Uppsala huko Sweden.
Televisheni ya al Jazeera imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, polisi wamewavamia waandamanaji hao ambao kwa mujibu wa katiba ya Sweden wana haki ya kuandamana kupinga ufedhuli wa mwanasiasa Rasmus Paludan wa kuchoma moto Msahafu.
Polisi wa Sweden wanaonesha kuunga mkono jinai hiyo ya Paludan lakini wakati huo huo hawawezi kuvumilia kuona watu wanalalamikia uhalifu huo. Polisi hao wamemtia mbaroni Muislamu mmoja aliyeshiriki kwenye maandamano hayo kwa sababu tu ya kusema Allahu Akbar.
Hii si mara ya kwanza Sweden kuruhusu kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kuchomwa moto nakala za Qur’ani Tukufu hadharani na mbele ya kamera za vyombo vya habari kwa madai ya eti uhuru wa kujieleza wakati ambapo anapotokezea Muislamu na kutamka tu Allahu Akbar hadharani kulalamikia jinai hiyo, wanamtia mbaroni.