Wakuu wa serikali ya Maldives wametangaza uamuzi wa kuwasomesha dini na Qur’ani raia wake waishio nje ya nchi, kwa njia ya Intaneti.
Mtandao wa habari wa AVAS umemnukuu Naibu Rais wa Maldives, Faisal Naseem, akitangaza habari hiyo Jumapili, Oktoba 11, 2020 alipoonana na wanaharakati wa kidini na kujadiliana nao njia za kuendesha masomo ya Kiislamu ikiwemo Qur’ani kwa njia ya Intaneti pamoja na lugha ya Dhivehi ambayo ndiyo lugha rasmi ya Maldives.
Amesema, raia wa Maldives waishio nje ya nchi ni wajibu wao kujua utamaduni wao, mafundisho ya dini yao na mila na desturi zao hasa wanafunzi wa vyuo vikuu. Amesisitiza kuwa, asasi zote husika zina wajibu wa kushirikiana na serikali kufanikisha jambo hilo la wajibu.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Waziri wa Elimu, Waziri wa Masuala ya Kiislamu na wawakilishi wakuu wa Kituo cha Taifa cha Qur’ani Tukufu cha Maldives. Nchi ya Maldives ni mjumuiko wa visiwa kadhaa. Iko kusini mwa India. Idadi ya watu wake ni takriban laki tano na 15,000. Zaidi ya asilimia 99 ya raia wa Maldives ni Waislamu. Raia takriban 25 elfu wa Maldives wanaishi nje ya nchi hiyo. Sehemu kubwa ya raia wa Maldives nje ya nchi, wako Sri Lanka, India na Malaysia.