Umoja wa Mataifa umetoa taarifa kwa mnasaba wa maadhimisho ya tarehe 21 Septemba ambayo inatambuliwa kuwa ni Siku ya Amani Duniani, na kusema kwamba mgogoro wa maambukizo ya kirusi cha corona ulimwenguni umetoa funzo kubwa kwamba mataifa ya dunia ni ndugu na si maadui.

Shirika la habari la SAWA la Palestina limenukuu taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa kwa mnasaba wa maadhimisho ya Septemba 21, Siku ya Amani Duniani ikisema: Leo hii adui wa mataifa yote ni kirusi cha corona ambacho ni tishio kwa usalama, amani na maisha ya wanadamu wote. Ugonjwa huu umeitumbukiza dunia yetu kwenye hali nzito na umetufunza kwamba tukio linapotokea katika kona moja ya dunia, linaweza kuiathiri dunia nzima.

Taarifa hiyo iliyotolewa kwa amri ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, imeashiria pia kwamba, miezi kadhaa iliyopita, Umoja wa Mataifa ulitoa mwito kwa pande zote zinazopigana duniani kuweka chini silaha zao na badala yake kuelekeza nguvu zao zote katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19 ambao haujawahi kutokea mfano wake na ambao umeshaenea dunia nzima.

Aidha Umoja wa Mataifa umewataka wanadamu wote kuwa na fikra moja na kubadilisha mawazo na taarifa katika kupambana na ugonjwa wa corona, ushirikiano ambao unaweza kuielekeza dunia kwenye mshikamano zaidi.

Kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Amani Duniani na ambayo inaadhimishwa leo Jumatatu Septemba 21, 2020, imeteuliwa iwe ni “Kupigania Amani kwa Pamoja.”

Aidha Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limetuma ujumbe maalumu kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku hii na kusema, utamaduni wa amani ni  utamaduni wa mazungumzo na kuishi kwa kuvumiliana  na kwamba jukumu la Umoja wa Mataifa katika suala hilo hivi sasa ni kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Mwaka 2001 Umoja wa Mataifa uliitangaza tarehe 21 Septemba kuwa Siku ya Amani Duniani kwa shabaha ya kuzuia machafuko na kuleta usimamishaji vita katika maeneo yenye vita na machafuko ulimwenguni.

(Visited 28 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!