Makundi makuu ya haki za binadamu kwa kushirikiaana na taasisi ya mavazi ya Kiislamu ya California nchini Marekani yameamua kuanzisha kampeni ya kuchapisha fulana (T-shirt) zenye maandishi ya hadhithi ya Mtume Muhammad SAW kuhusu uadilifu katika Uislamu na kupinga kwake kikamilifu dhulma na ubaguzi.
Hayo yameripotiwa na mtandao wa “About Islam” na kuongeza kuwa, zoezi la kushona fulana hizo limesimamiwa na Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu (CAIR) na juu yake kumechapishwa hadhiti maarufu ya Mtume Muhammad SAW kuhusiana na usawa wa wanadamu wote, bila ya kujali rangi, ukabila, taifa, lugha n.k.
Hadithi hiyo tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW inasema: “Wanadamu wote wanatokana na Adam na Hawa. Hakuna ubora wa Mwarabu juu ya asiye Mwaarabu wala asiye Mwarabu hana ubora wowote mbele ya Mwarabu. Aidha mweupe si bora kuliko mweusi na wala mweusi si bora kuliko mweupe. Mbora wenu ni mchaji Mungu zaidi na mwenye matendo mazuri zaidi.” Naibu Mkurugenzi Taifa wa taasisi hiyo ya CAIR, Bw. Edward Ahmed Mitchell amesema katika ujumbe wake kwenye Facebook kwamba, jamii yetu bado inateseka kwa historia ndefu ya ubaguzi wanaofanyiwa watu weusi na watu weupe, hivyo taasisi za Kiislamu zinapaswa kufanya kazi ya ziada ya kutia nguvu na kueneza maadili bora ya kuishi kwa kuvumiliana watu wa vizazi tofauti, kupiga vita ubaguzi na kufikisha vizuri ujumbe na mafundisho matukufu ya Mtume Muhammad SAW.