Athari kadhaa za sanaa za mkono za zama za kale za Uislamu ukiwemo ukurasa wa Msahafu wa zamani zaidi wa Qur’ani Tukufu katika Christie’s zitapigwa mnada mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba nchini Uingereza.
Toleo la mtandaoni la gazeti la al Sharq al Awsat limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, miongoni mwa athari hizo za sanaa za mkono za enzi za kale za Uislamu ambazo zitapigwa mnada katika mnada maarufu wa Christie’s mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba ni athari za Andalus, Misri, Syria, Iran, Afghanistan na India.
Miongoni mwa athari za thamani kubwa za kisanii katika mnada huo ni kinara cha kale cha taa za mishumaa kilichotengenezwa Mosul, Iraq katika karne ya Saba Milaadia, picha ya kuchora ya Mfalme Nasruddin Shah, vyombo vya enzi za wafalme wa kale wa Misri na kijisanduku cha mbao cha enzi za Bani Nasr huko Andalus.
Sara Plumbly, Mkuu wa Kitengo cha Sanaa za Kiislamu katika Mnada wa Christie’s amesema kuwa, ukurasa wa Msahafu wa zamani kabisa wa Qur’ani Tukufu utapigwa mnada mwishoni mwa mwezi huu. Amesema, athari hiyo ina thamani kubwa kihistoria na kidini. Ameongeza kuwa, Msahafu huo uliandikwa katika miaka ya awali kabisa ya Uislamu kwa kutumia Khat za Hijaz. Aidha amesema, hati za Msahafu huo zimeandikwa mbalimbali kwa mkono juu ya ngozi. Hivyo inaonesha Msahafu huo ulikuwa mkubwa sana.
Ni vyema tukasema hapa kwamba, Christie’s ni mnada maarufu sana wa sanaa duniani. Ofisi zake kuu ziko London na New York.