Katibu Mkuu wa Umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu amejibu matamshi yaliyo dhidi ya Uislamu yaliyotolewa na rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron aliyedai kuwa eti dini ya Kiislamu ni hatari kwa jamii ya Ufaransa.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu amesema, Uislamu ni dini imara na haina haja na nasaha za mtu yeyote yule.

Dk Muhammad bin Abdul Karim al Isa amesema hayo katika mahojiano maalumu ya televisheni na kusisitiza kuwa, Uislamu ni dini ya Mwenyezi Mungu, hivyo haiwezi kuyumbishwa na matamshi ya hapa na pale ya mtu huyu na yule.

Aidha amegusia jinsi Qur’ani Tukufu ilivyoamrisha kujiepusha na matamshi yanayoweza kuchochea kuchukuliwa misimamo hasi na kusema, tunakubali kwamba wako baadhi ya Waislamu wasioielewa dini ambao wana misimamo ya kuchupa mipaka inayokwenda kinyume na mafundisho ya dini yao, lakini hilo halipasi kutumiwa kuwaingiza Waislamu wote katika mkondo huo wa watu wachache wanaoharibu taswira ya dini kwa misimamo yao isiyo sahihi. Vile vile amewaasa Waislamu wasiunge mkono misimamo isiyo sahihi ya watu hao iwe kwa njia mubashara au isiyo ya moja kwa moja.

Dk al Isa ameongeza kuwa, wakati mtu yeyote anapojitokeza na kudai kuwa anakabiliana na misimamo mikali, tunapaswa kumwambia kwamba misimamo hiyo mikali hadi hivi sasa imewaletea matatizo mengi zaidi Waislamu na nchi zao kuliko maeneo mengine yoyote duniani. Hivyo ulimwengu wa Kiislamu ndio muhanga mkuu wa misimamo hiyo mikali na unapambana nayo. Kwa mantiki hiyo, asijitokeze mtu akajifanya kuwa yeye ndiye anayepambana au aliyedhuriwa zaidi na misimamo mikali.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anaendelea kulaumiwa vikali kwa matamshi yake ya chuki dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu. Rais huyo amezuka na mpango wa kuanzishwa sheria ya kuususia Uislamu akidai kuwa Waislamu takriban milioni 6 nchini Ufaransa eti ni tishio kubwa kwa jamii.

(Visited 17 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!