Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, ugonjwa wa COVID-19 maarufu kwa jina la corona umevuruga jitihada za kimataifa za kupambana na ugaidi na kuwasaidia wahanga wa matukio ya kigaidi.
Antonio Guterres aidha amesema huduma muhimu kama vile za kuutafuta njia za kisheria za kutoa misaada na kupigania haki za wahanga hao pamoja na kuwasaidia kisaikolojia zimevurugika. Pia amesema, janga la corona limekwamisha pia miaada iliyokuwa inatoka serikalini kwa ajili ya wahanga hao kutokana na juhudi kubwa za serikali hizo kuelekezwa kwenye vita dhidi ya COVID-19.
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameelezea kusikitishwa pia na jinsi mikutano ya kujadili masuala ya ugaidi ilivyozorota na kusauliwa wakati mikutano kama hiyo ni fursa kwa manusura kupata faraja. Amesema, baada ya kupita muda mrefu, iliamuliwa kufanyike mkutano kama huo, lakini hata mkutano huo nao umeakhirishwa hadi mwakani.