Waziri wa Wakfu wa Misri ametangaza habari ya kufunguliwa vituo 69 vya Qur’ani katika misikiti mikubwa ya nchi hiyo kwa ajili ya kulea vijana wanaohifadhi Qur’ani Tukufu na wanafunzi wa tajwidi.

Mtandao wa habari wa “Sada al Balad” umemnukuu Waziri wa Wakfu wa Misri, Mohamed Mokhtar Gomaa akisema hayo na kuongeza kuwa, vituo 69 vya Qur’ani vimefunguliwa katika misikiti mikubwa ya maeneo yote ya Misri kwa ajili ya hifdh na qiraa ya Qur’ani Tukufu ili kuhakikisha vijana hao wako chini ya maulamaa na maqarii bingwa katika malezi ya kiQur’ani ya hifdh na qiraa.

Waziri Gomaa ameongeza kuwa, vituo hivyo vimewekwa mbali na makundi yenye misimamo mikali ambayo yanatumia usomeshaji wa Qur’ani kama chaka la kuharibu fikra za vijana wadogo na kuwaingia kwenye magenge ya uhalifu.

Amma kuhusiana na muda wa masomo katika vituo hivyo, Waziri wa Wakfu wa Misri amesema, masomo ya awali katika vituo hivyo ni miaka miwili. Mwaka wa kwanza ni kwa ajili ya masomo ya awali ya Qur’ani Tukufu na hifdh pamoja na masomo ya hukmu za tajwidi.

Amesema, mwaka wa pili wa masomo katika vituo hivyo ni kwa ajili ya masomo ya juu zaidi kama vile kutia nguvu hifdh na qiraa yaani tajwidi katika vifua vya wanafunzi hao na pia kusomeshwa visomo mbalimbali vya Qur’ani, tafsiri, ulumul Qur’an na utamaduni wa Kiislamu.

(Visited 31 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!