Baraza la Taifa la Waislamu nchini Canada limetaka mauaji yaliyotokea katika msikiti mmoja mjini Torondo dhidi ya Muislamu mmoja yatambuliwe kuwa ni tukio la kigaidi kwani lilifanyika kutokana na hisia za chuki na ubaguzi.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti habari hiyo na kusema kwamba jeshi la polisi mjini Toronto limemtia mbaroni mtu mmoja kwa tuhuma za kumuua Muislamu mmoja katika msikiti wa Toronto. Sasa Baraza la Taifa la Waislamu nchini Canada limetaka mauaji hayo yatambuliwe kuwa ni ugaidi na ni uhalifu uliotokana na chuki za kidini.

Jana Ijumaa, Septemba 18, 2020, baraza hilo lilitoa tamko na mbali na kulishukuru jeshi la polisi la Toronto kwa kumtia mbaroni gaidi huyo kwa tuhuma za kumuua Muhammad Aslim Zafis (58), limetaka mauaji hayo yatambuliwe kuwa ni ya kigaidi yaliyotokana na chuki.

Tarehe 12 mwezi huu wa Septemba, Zafis alidungwa kisu na kujeruhiwa vibaya nje ya msikiti huo ambako alikuwa anafanya kazi ya kujitolea kuwasaidia wagonjwa wa COVID-19 msikiti hapo.

Jana Ijumaa, jeshi la polisi la Toronto lilitoa taarifa na kusema kuwa limemtia mbaroni mwanamme mmoja mwenye umri wa miaka 34 anayejulikana kwa jina la Guilherme “William” Von Neutegem na kumfungulia mashtaka ya mauaji ya daraja la kwanza.

Taarifa zinasema kuwa gaidi huyo alimvamia Zafis akiwa amekaa kitako juu ya kiti nje ya lango kuu la kuingilia msikiti humo na kumuua papo hapo kwa kumchoma kisu. Kwa mujibu wa televisheni ya al Jazeera, mauaji hayo yametokea baada ya baraza hilo la Waislamu mjini Toronto ambao ndio mji mkubwa zaidi nchini Canada kulalamika kwamba misikiti imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara mjini humo katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni.

(Visited 76 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!