Hasira za Waislamu katika kona mbalimbali za dunia zimeongezeka kwa ajili ya kumnusuru Nabii wa rehema, Mtume Muhammad SAW baada ya kuvunjiwa heshima huko Ufaransa.
Viongozi, maulamaa, watu muhimu na wananchi wa kawaida katika kona mbalimbali duniani wanaendelea kulaani kitendo cha kifidhuli cha kuvunjiwa heshima Bwana Mtume Muhammad SAW huku Rais Recep Tayyib Erdoğan wa Uturuki akimtaka Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akapimwe akili kutokana na matamshi ya kibaguzi aliyotoa hivi karibuni kuhusu dini tukufu ya Uislamu na kuunga mkono kuchapishwa tena vibonzo vinavyomtovukia adabu Mtume Muhammad SAW.
Rais Erdoğan amesema: “Hivi kwani Rais Macron wa Ufaransa ana tatizo gani na Uislamu na Waislamu? Mimi naona anahitaji kupewa matibabu ya matatizo ya akili.”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan ametuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kulaani matamshi ya kiuadui ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW nchini Ufaransa.
Ameandika: Kiongozi mwenye hekima ni yule anayewaunganisha watu kama alivyofanya Nelson Mandela, shujaa wa Afrika Kusini.
Hivi karibuni mwalimu mmoja wa historia nchini Ufaransa aliwaonesha wanafunzi wake picha za vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW. Raia mmoja kutoka Chechnya alimshambulia mwalimu huyo na kumuua. Tukio hilo linatumiwa vibaya na viongozi wa Ufaransa akiwemo Rais Emmanuel Macron aliyetoa maneno mabaya kuhusu dini tukufu ya Kiislamu na kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya Waislamu. Rais huyo wa Ufaransa pia ameunga mkono kitendo kiovu cha jarida la Charlie Hebdo cha kuchapisha tena vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW) na kusisitiza kuwa, Ufaransa itaendelea kuchapisha vibonzo hivyo. Macron amedai kuwa eti huo ni uhuru wa kujieleza.
Kwa upande wao Waislamu wa madhehebu ya Kishia nchini Lebanon kupitia baraza lao kuu wametoa tamko rasmi la kulaani kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW huko nchini Ufaransa.
Nayo Idara ya Wakfu ya Waislamu wa madhehebu ya Kisuni nchini Iraq pia imenukuliwa na shirika la habari la al Sumariya News ikilaani kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW huko Ufaransa wakisisitiza kuwa, Mtume Muhammad SAW ni nembo kuu ya Uislamu na kwamba kusambaza vibonzo vinavyomvunjia heshima, ni kuwakosea adabu Waislamu zaidi ya bilioni moja duniani.
Chuo Kikuu cha al Azhar cha nchini Misri pia kimenukuliwa na shirika la habari la “al Yaum al Sabi’i” kikiandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba Waislamu ni wahanga wa maneno yasiyo na maana ya wanasiasa wanaopigania kuchaguliwa tena katika nchi zao.
Dar al Fat-wa ya Jordan nayo imetoa tamko rasmi na kusema: Watu wanaomtovukia adabu Mtume Muhammad SAW hawamjui mtukufu huyo. Wanaonekana ni wajinga na hawaijui sira na mafundisho bora kabisa ya kibinadamu na ya kuishi salama kwa pamoja watu wote aliyokuja nayo mtukufu huyo wa daraja.
Kiujumla ulimwengu mzima wa Kiislamu umechachamaa kulaani utovu wa adabu aliofanyiwa Mtume Muhammad SAW nchini Ufaransa.
Hadi hivi sasa Kuwait imetoa onyo, Iran imelaani vikali jambo hilo, Jordan imesema, kitendo hicho cha Rais wa Ufaransa na wenzake kimewaumiza Waislamu wote duniani, makundi na taasisi mbalimbali pia zimelaani kitendo hicho kiovu na bado hasira za Waislamu zinaendelea kuoneshwa kwa sura mbalimbali duniani.