Makamu wa Kwanza wa Spika wa Bunge la Iraq ameitaka serikali ya nchi hiyo iitishe mkutano wa kimataifa wa maqarii wa Qur’ani Tukufu mjini Baghdad.

Hayo yameripotiwa na mtandao wa Ninanews ambao umemnukuu mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Bunge la Iraq akiitaka serikali ya nchi hiyo iwasilishe mpango wa kuitisha mkutano wa kimataifa wa maqarii wa Qur’ani tukufu kutoka kona zote za dunia hususan ulimwengu wa Kiislamu.

Sheikh Hassan al Kaabi ametoa mwito huo wakati alipokutana na mkuu na wajumbe wa Umoja wa Jumuiya na Makundi ya Qur’ani nchini Iraq na amewataka wakuu wa mikoa nchini humo watenge muda maalumu wa kusaidia na kuhamasisha shughuli za kidini. Amewashauri watumie wataalamu na watafiti katika masuala ya Qur’ani kufanikisha suala hilo.

Sheikh al Kaabi amezungumzia pia umuhimu wa Qur’ani Tukufu kwa wanadamu na viumbe wote na kusema kuwa, ni wajibu wetu kutekeleza kivitendo usia wa Bwana Mtume Muhammad SAW wa kuilinda na kushikamana na Qur’ani Tukufu kwa ajili ya kupata uongofu wa wanadamu. Amesema, moja ya mifano ya kukienzi na kukilinda Kitabu hicho cha Allah ni kuwajali maqarii wa Qur’ani popote walipo na kutumia mafundisho ya Kitabu hicho kitakatifu kukabiliana na mashambulizi makubwa dhidi ya Uislamu na Waislamu na dhidi ya Kitabu kitakatifu, yanayoendeshwa kila upande na maadui wa Mwenyezi Mungu duniani. Amesema, njia ya mazungumzo na maelewano ni mbinu nzuri ya kukabiliana na chuki, misimamo mikali na uenezaji chuki dhidi ya Uislamu.

(Visited 19 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!