Msikti na Kituo cha Kiislamu cha mjini New York Marekani kimejengwa kwa namna ya aina yake, ya kuchanganywa usanifu majengo wa kale wa Uthmania na wa kisasa na maeneo yake makuu kama vile mihrabu, ukumbi wa Sala na minara yamesanifiwa kwa muundo mzuri na wa kipekee kabisa.
Msikiti na kituo hicho cha Kiislamu kiko katika eneo la Harlem huko Upper Manhattan kusini mashariki mwa mji mkuu wa Marekani, New York. Huo ni miongoni mwa misikiti ya zamani kabisa mjini New York.
Mpango wa kujengwa kituo hicho ulianza mwishoni mwa miaka ya 60 Milaadia. Wakati huo ndipo ilipokuja fikra ya kuwa na kituo cha utamaduni wa Kiislamu kwa ajili ya Waislamu wa mji mkuu huo wa Marekani.
Hata hivyo fikra hiyo haikuweza kutekelezwa kivitendo kutokana na masuala kama ya kukusanya fedha zinazohitajika na mchakato mrefu wa kununua nyumba za eneo hilo, zoezi la kuvunja nyumba hizo n.k. Hatimaye ujenzi wa Msikiti huo ulianza mwezi Oktoba 1984.
Ujenzi wa ukumbi wa kusalia ulianza mwezi Mei 1987 sambamba na maadhimisho ya sikukuu ya Idul Fitr. Ujenzi wa ukumbi huo wa kusalia ulimalizika mwaka mmoja baadaye. Msikiti na Kituo cha Kiislamu cha New York Marekani kilifunguliwa rasmi tarehe 15 Aprili 1991 katika maadhimisho ya sikukuu ya Idul Fitr.
Ujenzi wa kituo hicho cha Kiislamu ambacho kinaweza kupokea Waislamu 1000 kwa wakati mmoja, uligharimu dola milioni 14 hadi kumalizika kwake.
Usanifu wa jengo la Msikiti wa kituo hicho umechanganywa baina ya ule wa zamani wa Uthmania na wa zama za hivi sasa. Maeneo ya asili ya Msikiti huo kama vile Mihrabu, ukumbi wa kusalia na minara, imesanifiwa kwa mvuto wa aina yake. Mbali na kutekeleza ibada ya Sala za kila siku, kituo hicho kinatoa huduma nyingi kama za masomo ya Kiislamu, ushauri nasaha, uandikishaji wa ndoa za Kiislamu, masuala ya mazishi, kukusanya zaka, kutoa misaada kwa wenye mahitaji n.k.