Matokeo ya uchunguzi mpya uliofanywa kwenye makanisa ya Ufaransa unaonesha ,kuweko idadi kubwa mno ya udhalilishaji wa kijinsia wa watoto wadogo na huo ni mgogoro mkubwa zaidi kuwahi kuripotiwa kwenye makanisa hayo katika kipindi cha karne tano zilizopita.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, uchunguzi mpya unaonesha kuwa, maelfu ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia wa watoto wadogo vimekuwepo kwenye makanisa ya Ufaransa tangu mwaka 1950.
Jean-Marc Sauvé, mkuu wa timu ya uchunguzi ililyoundwa kuchunguza vitendo hivyo, Jumapili, Oktoba 3, 2021, aliviambia vyombo vya habari kwamba, uchunguzi wa timu yake umebaini kuhusika maaskofu 2900 hadi 3200 wa makanisa ya Ufaransa katika na vitendo vya udhalilishaji wa kingono wa watoto wadogo wa kiume na kike.
Kwa mujibu wa Sauvé, idadi hiyo ya 2900 hadi 3200 ya maaskofu waliojihusisha na udhalilishaji huo ni ya chini kabisa kwani kuna uwezekano mkubwa wa idadi kubwa zaidi ya hiyo.
Uchunguzi huru ulianza kufanywa na Kanisa Katoliki la Ufaransa mwaka 2018 baada ya kufichuliwa kashfa nyingi kama hizo katika makanisa ya nchi nyinginezo.
Hii ni katika hali ambayo mwanzoni mwa mwaka huu, Papa Francis, Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani alibadilisha sheria za kanisa hilo ili kubana vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia hasa dhidi ya watoto wadogo.