Wanaharakati wa Palestina wametoa mwito wa Wapalestina wote, wajitokeza kwa wingi katika Sala ya Asubuhi ya Ijumaa ya wiki hii ya tarehe 11 Machi, 2022 itakayosadifiana na mwezi 8 Shaaban 1443 na kuutangazia ulimwengu kuwa kamwe hawatoutelekeza Msikiti wa al Aqsa na wataendeleza mapambano hadi watakapokikomboa Kibla hicho cha Kwanza cha Waislamu.
Kituo cha Upashaji Habari cha Palestina (PIC) kimewanukuu wanaharakati wa asasi za kijamii wakiwataka Wapalestina waendeleze harakati ya “al Fajr al Adhim” kwa kujitokeza kwa wingi sana katika Sala ya Alfajiri siku hiyo ya Ijumaa katika Msikiti wa al Aqsa kwa kauli mbiu ya لن نرحل – Kamwe hatutaondoka, ili kutangaza msimamo wao usiotetereka wa kukilinda Kibla cha Kwanza cha Waislamu na pia kufelisha njama za Israel na walowezi wa Kizayuni.
Harakati ya “al Fajr al Adhim” inaendelezwa kila Ijumaa kwa kaulimbiu maalumu inayohusiana na masuala muhimu ya Palestina, katika Msikiti wa al Aqsa.
Kwa mara ya kwanza harakati hiyo ya “al Faj al Adhim” ilianza kwenye mji wa al Khalil mwezi Novemba 2020 na lengo lake ni kukabiliana na hatari zinazoukabili Msikiti wa al Ibrahimi kutoka kwa Wazayuni.
Kupambana na njama za kubadilisha maeneo ya Wapalestina na kuyapa sura ya Kiyahudi, ni lengo jengine la harakati hiyo ya “al Fajr al Adhim.”
Mapambano hayo yanaendelea katika miji na maeneo yote ya Wapalestina hasa kwenye Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.