Baada ya shule za jimbo la Karnataka nchini India kupiga marufuku vazi la staha la Hijab, magenge yenye misimamo mikali ya Kibaniani na Kihindu yameyataka majimbo mengine ya India yafuate mkondo huo.
Mtandao wa habari wa TRT wa lugha ya Kiarabu umeripoti habari hiyo na kusema kuwa, magenge hayo yenye misimamo mikali ya Kihindu yameyataka majimbo mengine ya India yapige marufuku vazi la staha ya mwanamke wa Kiislamu Hijab na wametishia kuwashambulia Waislamu wanaofanya maandamano ya kupinga marufuku ya vazi hilo tukufu la Kiislamu.
Jumanne wiki hii, Machi 15, 2022, Mahakama Kuu ya jimbo la Karnataka huko India iliunga mkono uamuzi wa mwezi uliopita wa serikali ya jimbo hilo wa kupiga marufuku Hijab mashuleni. Siasa kuu za chama tawala cha Bharatiya Janata Party (BJP) ni kuondoa kabisa athari za Uislamu nchini India.
Magenge yote ya Kibaniani yenye misimamo mikali yamefurahishwa na marufuku hiyo na viongozi wao wanadai waziwazi kuwa hivi sasa wanaendesha kampeni ya kuhakikisha Waislamu hawaruhusiwi kuvaa Hijab mashuleni katika sehemu yoyote ile nchini India.
Ikumbukwe kuwa, hata kama Waislamu ni jamii ya wachache nchini India, lakini wanaunda moja ya idadi kubwa zaidi ya Waislamu duniani. Kwa mujibu wa Kituo cha Utafiti cha Pew, mwaka 2020, idadi ya Waislamu nchini India ilikuwa ni milioni 213 ambayo ni sawa na asilimia 15.5 ya wananchi bilioni 1.38 wa India.