Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al Azhar cha nchini Misri kimelaani mauaji ya wanawake wawili Waislamu waliokuwa wamevaa vazi la staha la Hijab na kusisitizia msimamo wake wa daima wa kupinga vitendo kama hivyo vya chuki na ubaguzi.
Mtandao wa habari wa “Arabi 21” umeripoti habari hiyo kwa kunukuu tamko rasmi lililotolewa na Chuo Kikuu cha al Azhar katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook. Tamko hilo limesema, al Azhar inalaani mauaji na ukatili dhidi ya mfuasi wa dini yoyote ile na kuwataka watu wote walaani vitendo vyote vya kigaidi bila ya kufanya ubaguzi wala kuangalia wahanga ni wafuasi wa dini gani.
Kimesema, kufuata siasa za kindumilakuwili na za kibaguzi mbele ya vitendo vya kigaidi kunachochea chuki na uadui baina ya wafuasi wa dini mbalimbali na kuwachochea magaidi kufanya jinai zaidi dhidi ya watu wasio na hatia.
Jumapili ya tarehe 18 Oktoba, 2020, wanawake wawili Waislamu wavaa Hijab kutoka Algeria walishambuliwa kwa visu na kuuliwa na magaidi wawili wanawake wazungu karibu na Mnara wa Eiffel huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa.
Jeshi la Polisi la Ufaransa limedai kuwa limewatia mbaroni wanawake wawili kwa tuhuma za mauaji hayo. Taarifa zinasema kuwa, wanawake hao wawili Waislamu waliouliwa kwa kudungwa visu mjini Paris, mmoja alikuwa na miaka 49 na mwingine alikuwa kijana zaidi; wote wawili wana asili ya Algeria.
Magaidi hao wanawake wazungu walisikika wakipiga mayowe wakisema: “Waarabu wachafu rudini nchini kwenu” na baadaye wakawadunga visu na kuwaua Waislamu hao bila ya sababu yoyote. Idadi ya Waislamu nchini Ufaransa ni zaidi ya milioni 5 na mara kwa mara wamekuwa wakikumbwa na vitendo kama hivyo vya mauaji ya chuki za kidini, unyanyasaji na ubaguzi.