Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia imetangaza kuwa, iko tayari kupokea Waislamu kwa ajili ya ibada za Hija na Umra kutoka nje ya Saudia.

Abdulrahman Shams, mwakilishi wa Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia amenukuliwa na “al Quds al Arabi” akitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, baada ya kufanikiwa kusimamia vizuri ibada za Hija na Umra kwa Waislamu waishio ndani ya Saudi Arabia, sasa wizara hiyo iko tayari kupokea mahujaji na watekelezaji wa ibada ya Umra kutoka nje ya Saudia.

Waislamu katika ibada ya Sala nchini Saudi Arabia

Amesema hayo Jumanne usiku, Oktoba 20, 2020 wakati alipohojiwa na kanali ya habari ya televisheni ya Saudi Arabia. Amegusia pia kwamba hadi hivi sasa Waislamu 45 elfu wameshafanya ibada ya Umra tangu iliporuhusiwa tena na kuongeza kuwa, tangu ilipoanza awamu ya pili ya Hija na Umra hadi hivi sasa Waislamu laki moja na 20,000 wameshashiri katika Sala za jamaa kwenye Msikiti Mtakatifu wa Makkah.

Alipouliza kuhusu namna Waislamu kutoka nje ya Saudi Arabia wanavyopaswa kujiandikisha kwa ajili ya ibada hizo, Shams amesema, Waislamu waishio nje ya Saudia wanapaswa kujiandikisha katika taasisi za kuaminika za masuala ya Hija na Umra. Amesema, Waislamu watakaoruhusiwa kuingia nchini Saudi Arabia kwa ajili ya Hija na Umra ni wale tu watakaokwenda kwa sura ya msafara. Mtu mmoja mmoja hatoruhusiwa kuingia nchini humo kwa ajili ya ibada hizo.

Matayarisho ya kupokea Mahujaji nchini Saudi Arabia

Aidha amewatahadharisha Waislamu wawe macho wasije wakatapeliwa na matapeli kama wale wanaodai kwamba mtu anaweza kujiandikisha kupitia application na simu ya mkononi ya “Iitamarna” akisisitiza kuwa, application hiyo ni maalumu kwa Waislamu wa ndani ya Saudia tu. Aidha amewatoa wasiwasi Waislamu na kusema kuwa, tangu iliporuhusiwa utekelezaji wa ibada za Hija na Umra na Sala za jamaa, hakuna kesi yoyote ya corona iliyoripotiwa. Hivyo Waislamu wanaotaka kutekeleza ibada za Hija na Umra ni lazima wapitie kwenye taasisi za kuaminika na waingie nchini Saudi Arabia kwa sura ya msafara ili protokali za kiafya ziweze kutekelezwa kama ilivyopangwa.

(Visited 29 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!