Baada ya Mahakama ya New Zealand kumuhukumu gaidi mzungu adhabu kali ambayo haijawahi kutolewa nchini humo kutokana na ukatili aliowafanyia Waislamu waliokuwa wanasali katika misikiti miwili mjini Christchurch, leo Ijumaa Waislamu kama kawaida wameendelea kusali katika msikiti wao wa al Noor lakini walipotoka wamekuta rundo la maua yaliyowekwa na wakazi wengine wa mji huo kuonesha mapenzi yao kwa Waislamu.

Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Brenton Tarrant gaidi mzungu ambaye aliwaua kwa umati Waislamu katika misikiti ya al Noor na Linwood mjini Christchurch amehukumiwa adhabu kali zaidi kuwahi kutolewa nchini New Zealand. Katika jinai hiyo, gaidi huyo aliua kwa umati Waislamu 51 na kujeruhi wengine 49 huku akionesha mubashara ukatili wake huo kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook.

Jinai hiyo imelaaniwa na kila mwenye hisia za binadamu duniani. Wananchi wa dini nyinginezo nchini New Zealand wameumizwa sana na mauaji hayo na mara kwa mara wamekuwa wakionesha hisia zao kwa njia tofauti kuwathibitishia Waislamu kuwa wanawapenda na hawana uadui nao. Ikumbukwe kuwa gaidi Brenton Tarrant ni raia wa Australia mwenye chuki mno na Waislamu.

Miongoni mwa hatua za kuonesha mapenzi zilizochukuliwa na wananchi wa dini nyingine huko New Zealand ni ya leo Ijumaa ya kukusanya maua mengi nje ya msikiti wa al Noor ambao ndicho kilichokuwa kituo kikuu cha mauaji ya gaidi huyo. Wamekusanya maua hayo kuonesha kufurahishwa kwao na adhabu kali iliyotolewa dhidi ya muuaji huyo katili. Akionesha kuguswa sana na hatua hiyo, Sheikh Jamal Foda, Imam wa Msikiti wa al Noor amewaambia waandishi wa habari kuwa sasa hivi utulivu umerejea nchini New Zealand na Waislamu sasa tunaweza kuishi kwa utulivu na wafuasi wa dini nyinginezo. Amesema raia wa New Zealand wana haki sawa na kwamba Waislamu na wasio Waislamu inabidi washirikiane kulinda amani na kujenga New Zealand iliyo bora.

(Visited 63 times, 1 visits today)
One thought on “Baada ya kusali Ijumaa, Waislamu waona msikiti umejaa maua”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!