Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na Chuo Kikuu cha al Azhar cha nchini Misri kimetoa taarifa tofauti za kulaani kuchomwa moto nakala ya Qur’ani Tukufu katika mji wa Malmö nchini Sweden, taarifa zilizosema kuwa kitendo hicho ni cha kichokozi na cha kuchochea hasira za Waislamu.

Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, leo Jumapili, Agosti 30, 2020, jumuiya ya OIC imetoa taarifa na kulaani kuchomwa moto nakala ya Qur’ani Tukukfu huko Sweden.

Taarifa ya OIC imesema kuwa, kuchoma moto nakala ya Qur’ani Tukufu ni uchochezi wa wazi ambao lengo lake hasa ni kupiga vita juhudi za kimataifa za kupambana na taasubu, chuki na kutochochea hisia za kidini za watu wengine. Vile vile jumuiya ya OIC imeipongeza serikali ya Sweden kwa kuwatia mbaroni maadui hao wa Uislamu na kupinga rasmi vitendo vya kichochezi wanavyofanyiwa Waislamu.

Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri

Taarifa ya al Azhar

Chuo kikuu cha al Azhar cha Misri nacho kimetoa taarifa kali ya kulaani kuchomwa moto nakala ya Qur’ani Tukufu kulikofanywa naadui wa Uislamu, Ijumaa usiku katika mji wa Malmö wa kusini mwa Sweden wakati wa maandamano ya wabaguzi wa rangi wengi chuki na Uislamu na Waislamu.

Al Azhar imesema, kitendo hicho cha wabaguzi hao wa rangi huko Sweden kinakinzana na madai ya kuweko uhuru wa kila mtu kuwa na itikadi ya dini anayoona inafaa na kuishi kwa kuheshimiana. Ikumbukwe kuwa kuruhusiwa vyombo vya habari vya Magharibi kuonesha sura isiyo sahihi kuhusu Uislamu nako kunachochea fikra za kuwavunjia heshima Waislamu na matukufu yao.

Msimamo wa Jihadul Islami ya Palestina

Kwa upande wake Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina nayo imetoa taarifa ya kulaani kuchomwa moto nakala ya Qur’ani Tukufu nchini Sweden na kusema hiyo ni jinai.

Taarifa ya Jihadul Islami ya Palestina imesema, kitendo cha watu waovu cha kuchoma moto nakala ya Qur’ani Tukufu huko Malmö, Sweden kinatokana na fikra za kigaidi na ni kitendo cha kuchochea kwa makusudi hasira za Waislamu.

Itakumbukwa kuwa licha ya polisi wa Sweden kupiga marufuku maandamano ya watu wenye chuki za kidini, lakini genge moja la watu hao lilijitokeza barabarani Ijumaa usiku na kuchoma moja nakala moja ya Qur’ani Tukufu katika mji huo wa Malmö wa kusini mwa Sweden na baadaye kusambaza mitandaoni video ya jinai yao hiyo.

Polisi wa Sweden walifika kwenye eneo hilo na kuwatia mbaroni watenda jinai hao. Fujo zilitokea wakati wa operesheni ya kutiwa nguvu maadui hao wa Uislamu.

(Visited 15 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!